Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania(NBAA) imeendelea kutoa elimu na kujenga ufahamu juu ya Taaaluma ya Uhasibu kwa wanafunzi wa vyuo na shule mbalimbali za sekondari nchini.
Kwa kipindi hiki NBAA imetembelea mkoani Tanga ikiwa na lengo la kuwajengea ufahamu wanafunzi kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo Afisa Masoko na Mawasiliano Mwandamizi wa NBAA, Magreth Kageya amesema lengo la ziara hizo ni kuwahamasisha wanafunzi walioko shuleni hasa shule za Sekondari na vyuoni kupenda na kusoma masomo ya Uhasibu.
Pia amesema si kila aliyesomea uhasibu anaweza kufanya kazi za kihasibu bali inabidi kufanya mitihani ya Bodi hiyo ili kupewa cheti cha kitaaluma ili aweze kutambulika kama Mhasibu na kuweza kufanya kazi nje na ndani ya nchi.
Naye Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka ametoa elimu kwa wanafunzi kuhusu hatua wanazoweza kupitia ili kuweza kufikia kwenye hatua ya kupata cheti cha Taaluma yaani CPA.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni ATEC I na ATEC II kwa ngazi ya watunza vitabu na Foundation, Intermidiate na Final kwa ngazi ya Taaluma.
Afisa Masoko na Mawasiliano Mwan wa NBAA, Magreth Kageya akitoa elimu kuhusu kazi zinazofanywa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nguvumali iliyopo mkoani Tanga.
Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Nguvumali Venosa Massawe akiwatambulisha na kuwakaribisha wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kuwahamasisha wanafunzi hao kujiunga na masomo ya Uhasibu watakapomaliza masomo yao ya Sekondari.
Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nguvumali pamoja na kuwahamasisha wanafunzi hao kujiunga na masomo ya Uhasibu watakapomaliza masomo ya Sekondari.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nguvumali wakifuatilia wataalamu kutoka NBAA waliokuwa wanatoa elimu shuleni hapo