Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Shirika lisilo la Serikali la UWEZO TANZANIA limelenga kutafuta ufumbuzi wa Changamoto zinazowakabili vijana katika kupata stadi za maisha ili waweze kuwa na maarifa na uwezo wa kuishi katika misingi bora inayokubalika na jamii.
Mkurugenzi wa shirika hilo la UWEZO TANZANIA Baraka Mgohamwende amesema hayo katikak Mkutano uliohusisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa mashirika yasiyo ya Serikali, walimu, na wazazi, kwa lengo la kujadili maendeleo yaliyopatikana na kupanga hatua za mbele kwa mwaka 2025.
Amefafanua kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mtandao wa RELI AFRIKA wamefanya, Utafiti ambao umeonesha asilimia nane ya vijana wanaweza kutatua changamoto zao wenyewe zinazoweza kuwakabili.
Ameeleza kwamba utafiti, ulihusisha Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara kwa kufikia Wilaya 35 na kuwafikia vijana 17000 ambapo umahiri wa vijana katika stadi za maisha kwa kushirikiana na kutatua changamoto unaonesha kiwango cha umahiri kipo chini.
“Sasa tunatafuta muarobaini wa kuweza kupandikiza kukuza umahiri kwa vijana waweze kujisaidia wenyewe na kuweza kutumika vizuri kwenye jamii, kwa kushirikiana na taasisi ya elimu Tanzania na wadau wa chuo kikuu cha Dar es salaam tunaandaa namna ya kupima ubobevu wa vijana katika hilo eneo kwa kushirikisha mifumo ya serikali Ikiwemo ushirikishwaji wa walimu pamoja na wazazi katika kuleta malezi bora,” alieleza.
Aliongeza kusema kuwa wameanza na vijana wa miaka 6 mpaka miaka 17 waliopo katika shule za msingi na shule za sekondari na kushirikisha vijana walio nje ya shule ambao hawakupata fursa ya kuwa shuleni ama kuacha kuhudhuria masomo.
Alifafanua kwamba, wamewaleta pamoja wadau mbalimbali wanaofanya kazi katika mradi huo ikiwemo Wizara mtambuka Ofisi za NGO’s kupitia kwa pamoja kuona namna gani wanaweza kuwa natija katika kuboresha na kushirikisha wadau wengi zaidi.
Kwa upande wake, Digna Mushi, ambaye ni Kiongozi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (RELI), amesema kuwa kupitia ripoti ya utafiti huo, watatengeneza mikakati madhubuti kuhakikisha kuwa vijana na watoto wanapata ujuzi wa kushirikiana na kuwasiliana ili waweze kujitatulia changamoto zao.
“Mradi huu umeangazia namna walimu na wazazi wanavyowatengeneza watoto wenye uwezo wa kushirikiana na kuwasiliana. Sasa kupitia mkutano huu, tutachakata maoni na kuweka mkakati mahususi wa kufanikisha lengo hilo,” amesema Digna
Naye Mahmudi Ngamange, Afisa Ubora wa Elimu wa Shirika la SAWA, amesema kuwa mradi huo umeleta mafanikio makubwa katika Wilaya ya Mvomero, Morogoro, hasa katika kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Kwa mfano, kupitia mradi huu tuliwafundisha wazazi nao wakawafundisha watoto wao namna ya kuchunga mifugo bila kuharibu mashamba ya wakulima. Mafunzo haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro baina yao,” amesema Ngamange.
Mkutano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuboresha elimu ya stadi za maisha na maadili nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.