Na Masanja Mabula, PEMBA.
BARAZA la Wawakilishi Zanzibar ndio chombo chenye mamlaka ya kutunga na kuzirekebisha sheria ambazo zinaonekana kupitwa na wakati pamoja na zile kandamizi zinazonyima uhuru wa baadhi ya makundi.
Zipo sheria ambazo Baraza la Wawakilishi limetunga ambazo zinakwaza uhuru wa Habari na uhuru wa kujieleza kama Kifungu cha 30 kinachompa mamlaka makubwa Waziri wa Habari kufungia chombo cha Habari.
Aidha zipo pia taasisi nyingine ambazo kazi yake ni kufanya ushawishi kwa mamlaka za kutunga sheria ili kuziondoa baadhi ya sheria ambazo zinakinzana na sheria mama ambayo ni Katiba ya nchi.
Kuwepo na sheria kinzani kumewafanya wadau wa habari pamoja na waandishi wa habari kupaza sauti zao kuomba baadhi ya sheria kuondoshwa ama kufanyiwa marekebisho ili ziendane na wakati wa sasa.
Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 18 kimetoa uhuru wa kutoa maoni, kutafuta, kutoa habari, kupata na kusambaza habari lakini baadhi ya sheria hazikubaliani na kifungu hichi cha Katiba.
Katika kifungu 18 (1) kimeeleza kuwa “ bila ya kuathiri sheria nyengine za nchi, kila mtu anayo haki na uhuru wa kutoa maoni (kujieleza) kutafuta, kupokea na kusambaza habari na mawazo yake kupitia chombo chochote cha Habari bila ya kujali mipaka ya nchi na pia anayo haki na uhuru wa kutoingiliwa mawasiliano yake”
Kumekuwapo jitihada mbali mbali kutoka kwa wadau wa habari pamoja na waandishi wa habari wanaotaka baadhi ya sheria zifanyiwe marekebisho ili kuviondoa vifungu kandamizi ambavyo vinapinga wazi wazi uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Imekuwa ni kipindi kirefu sasa tangu sauti za wadau wa habari na waandishi wa habari zilipoanza kusikika wakilalamikia kuendelea kutumika kwa sheria ambazo haziendani na matakwa ya Katiba kuwa kushauri muswada wa sheria ya huduma za habari upelekwe katia Baraza la Wawakilishi usomwe , ujadiliwe na hatimay upitishwe kua sheria mpya ya habari wakiaminikuwa utakuwa mwarubaini wa changamoto zinazowakabili.
Bado kilio na sauti hizo za wadau wa habari na waandishi wa habari hakijapatiwa ufumbuzi unaofaa licha ya mamlaka husika kukisikia kilio hicho ambacho kinazidi kuwadhoofisha huku wakiwa hawajui la kufanya.
Ni takribani miaka mitatu iliyopita ambapo wadau wa habari na waandishi wa habari walijawa na furaha wakiamini kuwa kilio chao kinakwenda kupata wa kuwafuta machozi, baada ya Serikali kuanza mchakato wa kupitisha sheria ya habari.
Mikutano mbali mbali ya wadau wa habari pamoja na makongamo yamefanyika kwa lengo la kukusanya maoni ya rasimu ya sheria ya habari, ambapo waandishi wa habari pamoja na wadau wa habari walijawa na matumaini kwamba huo ndio mwanzo mzuri kuelekea kupata sheria mpya ambayo itakuwa mwarubaini wa sheria zinazokwamisha uhuru wa habari.
Mtetezi wa haki za binadamu Tatu Abdalla Msellem ameiambia Makala haya kuwa kuchelewa kupitishwa kwa sheria ya habari kunazidi kuwanyima uhuru waandishi wa habari pamoja na wadau wa habari kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Ameshauri mamlaka kuwa na jicho la tatu kwa kuangalia gharama zilizotumika kuandaa rasmu hiyo kwa kuandaa mikutano na makongamano mbali mbali ili kukusanya maoniya wadau lakini mpaka sasa ni kama jitihada hizo zimepotea bure.
“Hili ni tatizo la kiuchumi, fedha nyingi za Serikali zimetumika katika kukusanya maoni ya rasimu ya sheria ya habari, kwa hiyo kushindwa kupitishwa pia ni sawa na kuziangamiza fedha za walipa kodi wa nchi hii,” amesema Tatu.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, sheria ya habari kama itapitishwa itawasaidia sana waandishi wa habari kuletekeleza majukumu ya kazi zao kwani watakuwa huru kuihabarisha jamii kwa kufuata misingi ya taaluma yao.
“Unajua mwandishi hata sisi watetezi wa haki za binadamu tunapata tabu kwani waandishi wanashindwa hata kuandika habari za uchunguzi wakihofu sheria kuwakandamiza,” amefahamisha.
Naye mwandshi wa habari mkongwe Zanzibar Farouk Karim amesema kuchelewa kupitishwa kwa sheria ya habari Zanzibar pia kunakwamisha ajira kwa vijana.
Amesema kuwa wapo vijana wengi waliosoma taaaluma ya habari na ambao kwa sasa wako mitaani wakisubiri sheria ipitishwe waweze kujiajiri kwa kuanzisha mitandao ya kijamii.
“Hii hali pia iko kiuchumi kwani inakwamisha uanzishwaji wa vyombo vya habari, kwani jamii inashindwa kuanzisha kwa hofu ya kuwepo na sheria iliyompa mamlaka makubwa Waziri wa kukifungia chombo cha habari anapohisi kuna haja ya kufanya hivyo,” amesema.
Farouk amesema kifungu cha Waziri kuweza kufungia chombo cha habari hakina afya kwa tasnia ya habari, jukumu hili linapaswa kuwa la mahakama na sio Waziri wa Habari.
Akizungumzia rasimu wa sheria ya habari, Farouk amesema kuwa pamoja na kwamba haiwezi kuzindoa changamoto zote kwa pamoja lakini itapunguza na kuongeza uhuru wa habari.
“Unapoomba shilingi mia moja ukapewa shilingi sabini utakuwa umepunguza kwani kwa kiasi Fulani utakuwa umeweza kutatua shida zako, na hii sheria ya habari sio kwamba inaziondoa changamoto zote moja kwa moja lakini tuna imani kuwa itakwenda kupunguza…” alisema Farouk..
Mwanasheria wa kujitegemea Khamis Shoka Ame amesema ni kweli kuchelewa kupitishwa Sheria ya Habari Zanzibar, kunazidi kuwanyima uhuru wadau na waandishi wa habari kutokana na kuwa sheria ya sasa imepitwa na wakati.
Ameongeza kuwa Sheria ya habari ya sasa ina mapungufu mengi likiwemo lile la Waziri kupewa mamlaka makubwa ambayo kama atayatumia vibaya, yanaweza kuathiri uhuru wa habari na kazi za waandishi wa habari kwa ujumla.
Aidha amesema iwapo sheria ilipaswa ibainishe vipengele ambavyo vinaweza kutumiwa na Waziri kufanya maamuzi ya kufungia chombo cha habari, na isitumike kwa ajili ya kulinda dhana ya maslahi ya Umma.
“Napendekeza au nashauri kuundwe bodi ambayo mwenyekiti wake awe na sifa ya kuwa mwandishi wa habari, ambaye ataweza kumshauri Waziri kulingana na misingi na taaluma ya habari kufanya hivyo naamini waandishi mtakuwa salama katika kazi zenu,” amedokeza.
Naye Ali Mbwana Khatib mmiliki wa JT online TV amesema pamoja na kuitikia wito wa Serikali wa kujiajiri, lakini anashindwa kuajiri kwa kuhofoa Sheria iliyopo, maana hajui Waziri ataamka vipi na hivyo anashindwa kutoa huduma bora kwa jamii.
“Mara ya kwanza niliposikia sheria inabadilishwa kwa kweli nilifurahi kwani niliamini ukombozi wa waandishi wa habari na wadau wa habari umefika, lakini mpaka sasa tumebaki kwenye wingu zito,” amefahamisha.
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar Dk Mzuri Issa akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari mwaka 2024 alisema mchakato huo umeanza zamani lakini mpaka sasa umeshindwa kukamilika.
Amesema kwa kipindi chote hicho wadau wa vyombo vya habari Zanzibar wamekuwa wakipaza sauti kuiomba Serikali ikamilishe mchakato huo wa marekebisho wa Sheria za Habari zilizotolewa maoni na wadau ili kutoa mazingira rafiki kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila ya vikwazo.
“Sisi wengine tangu tukiwa waandishi wa habari chipukizi tunazungumzia kupata sheria mpya za habari, tangu 2008 kwa kweli ni muda mrefu, tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimaye tupate sheria mpya ya habari Zanzibar,” amesisitiza.
Anasema kuwa, hatari ya kifungu hicho cha 30 cha sheria ya Wakala wa Habari, Magazeti na vijarida na. 5 ya mwaka 1988 ni kule kumpa Waziri mamlaka ya kufungia gazeti kwa maslahi ya taifa anapoona inafaa. Waziri anaweza kuyatumia vibaya mamlaka hayo kwa maslahi binafsi au ya kisiasa.
Januari 18, 2024 kamati ya wadau wa habari Zanzibar ZAMECO ilikutana kujadili masuala yanayohusiana na maendeleo ya sekta ya habari, changamoto na hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza sekta hiyo ambayo ni muhimu katika ujenzi wa jamii inayozingatia usawa na misingi ya utawala bora na demokrasia.
Kikao hicho maalum kilijadili kwa kina changamoto za sheria za habari Zanzibar ambazo ni kandamizi na hatua zilizochukuliwa na wadau wa habari ambao walitoa maoni yao hususan katika kufanya uchambuzi wa kina wa sheria hizo zinazokwaza waandishi wa habari kufanya majukumu yao kwa ufanisi.
“Tunapongeza na kushukuru wadau na serikali kwa jinsi walivyoibeba ajenda hii muhimu na kwa ahadi yake kupitia kauli na matumaini ya viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Rais Mhe Dk Hussein Ali Mwinyi ambaye alieleza wakati wa kutimiza siku 100 za Urais wake kwamba atahakikisha sheria mpya ya habari inapitishwa lakini hadi sasa ambapo ametimiza miaka mine ya kuwepo madarakani lakini sheria hizo hazijarekebishwa.
Ni matumaini ya wadau na waandishi wa habari kuwa mwaka 2025 ndio kipindi muafaka na sahihi kuhakikisha lengo la kuwapo sheria mpya ya habari Zanzibar ambayo itakuwa rafiki kwa waandishi wa habari kwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi linafikiwa.
Waandishi wa habari Kisiwani Pemba wajadili jambo kuhusu na sheria ya habari ya habari ambazo zinapinya uhuru wa habari
Mkutano wa waandishi wa habari kuhusu sheria ya habari zanzibar katika ukumbi wa Mikutano ya Ofisi za Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania-TAMWA Ofisi ya Pemba.