Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imefanya ziara ya uhamasishaji na uelimishaji katika vijiji vya Nsongwi Juu, Nsenga na Mbeye1, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uhusiano na jamii zinazouzunguka mradi wa Jotoardhi Ngozi.
Uhamasishaji na uelimishaji huo ni katika kuimarisha ushirikiano, ulinzi na umilikishwaji wa miradi kwa wananchi na kuwafanya waitunze na kuipa kipaumbele cha utunzaji katika sehemu iliyopita mradi wa jotoardhi Ngozi,
Ziara hiyo imefanyika kuanzia Machi 17 hadi 20, 2025 kwa nyakati tofauti ambapo wakazi wa maeneo hayo wamenufaika na elimu iliyotolewa na kuonesha utayari wao katika kuipokea na kuilinda miundombinu inayozunguka miradi ya jotoardhi.
Wataalam kutoka TGDC Khadija Ahmed, Mhandisi Luhinda Luyagwa, Mhandisi Esther Range, Juma Mpamba, Boaz Mazigo, Joshua Nelei, Omary Seleman na Leonce Komba walitoa elimu kwa wakazi wa vijiji hivyo vitatu.
Taarifa ya TGDC kwa vyombo vya habari imeeleza wametoa elimu kuhusu ufahamu na umuhimu wa utunzaji wa mradi pindi shughuli za uchimbaji zitakapoanza kwa ajili ya uhakiki wa rasilimali ya jotoardhi ikiwa ni safari kuelekeza uzalishaji umeme utokanao na rasilimali ya jotoardhi.
Pia wamesisitiza umuhimu wa wananchi kuiona miradi na miundombinu yote iliyowekwa na itakayowekwa kama miradi yao wakiilinda na kwakuwa inatekelezwa na Serikali itawanufaisha wananchi wote wakiwemo wa maeneo yanayozunguka mradi, hivyo wanapaswa kuilinda.
Pamoja na mengine, waliahidiwa kuwa sehemu ya watekeleza mradi kupitia ajira zitolewazo kwa kuzingatia wazawa ikiwemo vibarua, walinzi wakati utekelezaji utakapoanza.
Wataalam hao wamewaomba kila mmoja kuwa mlinzi wa mazingira kwa kuwa miongoni kwa kampeni ya TGDC ni utunzaji wa mazingira na hata umeme wa jotoardhi utakapozalishwa utakuwa ni rafiki wa mazingira. Pia waliombwa kuwa na mawasiliano ili inapotokea changamoto yoyote basi iwe rahisi kutatuliwa.
Kwa upande wa wananchi wa Nsongwi Juu, wameishukuru TGDC kwa elimu iliyotolewa na walihitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo ni kwa jinsi gani wazee wenyeji walivyoyatunza mazingira watanufaika na mradi, utoaji vipaumbele vya ajira kwa wazawa na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, mambo ambayo yalitolewa ufafanuzi kwa kuhakikishiwa ajira pamoja na uboreshaji wa barabara.
Wananchi wa Kijiji cha Nsenga nao waliuliza kuhusu namna ya kunufaika na mradi ikiwemo ajira kwa vijana, pamoja na miundombinu ya barabara, jambo ambalo lilitolewa ufafanuzi na kuhakikishiwa ajira za muda wakati wa utafiti na za moja kwa moja wakati wa uzalishaji, uboreshwaji miundombinu pamoja na mashirikiano baina ya TGDC na wananchi
Wakati Kijiji cha Mbeye 1 wameishukuru TGDC kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono shughuli za jamii ya wana Mbeye1 ikiwemo kupeleka maji katika Shule ya Msingi Mbeye1, jambo lililowapunguzia ajali wanafunzi waliokuwa wakivuka barabara kwa ajili ya kufata maji. Pia ugawaji mabegi kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na vifaa kama daftari.
Katika hatua nyingine, wana Mbeye1 wamelaani uharibifu wa miundombinu ambao hufanywa na watu wasiowaaminifu na wao kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuilinda miundombinu ya TGDC, huku wakiiomba TGDC kuendelea kuishika mkono kwenye ujenzi wa zahanati na madarasa ya shule na miundombinu ya barabara.
Kutokana na maelekezo hayo wataalam wa TGDC waliahidi kuyashughulikia kwa ukaribu katika kuyajadili katika ngazi ya maamuzi.
Pamoja na hayo TGDC imeeleza kuwa iko mbioni kuhakiki rasilimali ya jotoardhi katika miradi ya kipaumbele mitano ya Ngozi na Kiejo-Mbaka (Mbeya), Songwe (Songwe), Luhoi (Pwani) na Natron (Arusha) yenye lengo la kuzalisha Megawati 200 za umeme ifikapo 2030.
Kwa sasa itaanza na mradi wa jotoradhi Ngozi (70Mw) ambapo baada ya uhakiki, hatua ya uzalishaji itafuata.Na kwa kufanya hivyo TGDC itakuwa imechangia umeme kwenye gridi ya Taifa unaotokana na nishati safi isiyoharibu mazingira.