Jumla ya Gramu 3263.72 za dhahabu zenye thamamani ya shilingi milioni 749,509,531.94 zimekamatwa zikisafirishwa kinyume cha sheria mkoani Geita.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu waliokamatwa wakiwa na dhahabu hizo wakisafirisha kwa njia za magendo pia kinyume cha sheria kwa kutumia gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T.739 EEH mali ya Emanuel Kidenya Mkazi wa Kahama, Shinyanga.
Waliokamatwa ni Yohana Idama (34), Mkazi ya Nyamhongolo wilaya ya Ilemela Mwanza, Moshi Manzili (26), Mkazi wa Bariadi Simiyu na Hamidu Salum (25), Mkazi wa Nyasubi wilaya ya Kahama Shinyanga.
Watuhumiwa hao wamekamatwa Machi 24, 2025 majira ya saa 5 usiku katika Mtaa wa Kapera Wilayani Bukombe baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za siri na kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hawa. Baada ya upekuzi wa gari kufanyika, walikutwa wakiwa na kiasi hicho cha dhahabu kilichokuwa kimefichwa ndani ya gari hiyo.
Uchunguzi wa tukio hili kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine unaendelea kufanyika sambamba na kubaini na kuwakamata watakaobainika kujihusisha na uhalifu huo na kuwafikisha Mahakamani mara moja.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kujihusisha na vitendo vya magendo na biashara haramu kwani halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.