Na: Calvin Gwabara – Arusha.
Mwandishi Mkuu wa sheria nchini
Tanzania Bwana Onorius John Njole amewakumbusha Mawakili wa serikali nchini
kuzingatia Katiba ya nchi wanapoandika sheria au wanapotoa ushauri wa kisheria
kwa serikali katika jambo lolote.
Mwandishi Mkuu wa sheria nchini Tanzania Bwana Onorius John Njole akiwasilisha mada yake mbele kwenye mkutano huo jijini Arusha. |
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria
ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya pili ya mwaka ya Mawakili wa serikali
nchini yanayoendelea Jijini Arusha na kuwakutanisha zaidi ya Mawakili 300
kutoka kila kona ya Tanzania.
“Katiba iongoze ushauri wowote
mnaoutoa kwa Serikali katika jambo lolote linalohitaji ushauri wa kisheria
kutoka kwenu kama Mawakili wa Serikali, lakini pia huwezi kuwa mshauri mzuri wa
kisheria kama hujui mambo ya Muungano” alisisitiza Njole.
Aliongeza “Pamoja na kuwa mnatoa
ushauri na Tafsiri kwa mujibu wa sheria kwa Serikali lakini lazima kuzingatia
Sera, Mazingira na Ajenda za nchi na
dunia kwa wakati huo”.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria
nchini amesema kwa sasa Serikali inahamasisha uwekezaji kwahiyo unapoletewa
jambo utoe ushauri wakati unajua kuwa linakinzana na sera ya wakati huo sio
vyema kuishia kusema kuwa sheria hairuhusu bali toa ushauri wa nini kifanyike
kurekebisha sheria husika kama litakuwa na maslahi mapana kwa Taifa.
Bwana Njole amewasa mawakili hao
wa serikali wanapotoa ushauri kwa kusema jambo fulani ni hatarishi kwa
maendeleo ya nchi, basi ni vyema pia kusema namna ya kuzitatua ili tupate tija
lifanyike kwa tija bila kuleta athari kwa nchi.
“Nyinyi kama Washauri wa Serikali
kwenye masuala ya kisheria kwenye maeneo yenu lazima umjue mnayempatia ushauri,
acheni kuandika maneno magumu na kuzunguka zunguka kwa maneno mengi, weka
ushauri wako mwanzo tuu wakati mnashauri Mawaziri, Makatibu wakuu na viongozi wengine
maana wana kazi nyingi hawawezi kuanza kusoma taarifa ndefu sana” alihimiza
bwana Njole.
Akichangia mada hiyo Jaji Mstaafu wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu, Mhe.
Sirillius Matupa amewataka mawakili wa serikali hao wanapotoa ushauri wa
Kisheria kama Wakili wa Serikali kuhakikisha ushauri wanaoutoa haupigi kelele.
“Mnapopewa jukumu la kutoa
ushauri wa kisheria kwa serikali kuhusu jambo lolote hakikisheni ushauri
mnaoutoa haupigi kelele, maana tumeshuhudia nyakati fulani unapokea ushauri
kutoka kwa mtaalamu wa sheria lakini kunakuwa na malalamiko na maneno mengi
sana kuhusu ushauri huo na hivyo kusababisha mtoa maamuzi kupata shida kwenye
kuutumia” alisema Mhe. Jaji Mstaafu Matupa.
Mafunzo hayo ya siku tano yanawakutanisha
mawakili wa serikali kutoka kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la
kuwajengea uwezo na kuwakumbusha mambo mbalimbali ambayo wanapaswa kuyazingatia
wakati wanatekelez majukumu yao ili waweze kutoa mchango chanya kwenye
maendeleo ya taifa.
MATUKIO KATIKA PICHA KWENYE MKUTANO WA BESPOKE2025
Mwanasheria mkuu wa serikali Mhe. Hamza Johari (Katikati) akifuatilia mada kwenye mkutano huo, kushoto kwake ni Mwandishi Mkuu wa Sheri CPD Bwana Onorius John Njole. |