Dar es Salaam, 27 Machi 2025. Bahati Nasibu ya Taifa ya Tanzania leo imesaini ushirikiano na jukwaa bora la huduma za kifedha kwa njia ya simu hapa nchini, Vodacom M-pesa, Ili kurahisisha miamala ya bahati nasibu ya Taifa na kupanua fursa za kibiashara kupitia mfumo wa fedha wa kidijitali.
Kuunganishwa kwa bahati nasibu ya Taifa kwenye jukwaa la M-Pesa, kutawapa watumiaji urahisi wa upatikanaji wa michezo ya bahati nasibu kupitia jukwaa salama.
Kwa kutumia mtandao mpana wa Vodacom wenye zaidi ya watumiaji milioni 26, ushirikiano huu utawezesha urahisi wa ununuzi wa tiketi za michezo ya kubahatisha, kupitia majukwaa ya kidijitali ya Vodacom, ikiwemo huduma za M-pesa kwa njia ya simu, USSD codes na aplikesheni ya M-pesa.
Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania, Kelvin Koka, ameelezea ushirikiano huu kuwa ni hatua kubwa katika sekta ya michezo ya kubahatisha nchini. “Ushirikiano huu na M-Pesa utahakikisha kwamba wachezaji wanashiriki kikamilifu katika michezo ya bahati nasibu, huku ukihamasisha wafanyabishara kuweza kushirikiana nasi kwa kuwa jukwaa letu linazingatia uwazi na mustakabali ujao wa bahati nasibu ya Taifa. Kwa kuwa M-Pesa ni mshirika wetu rasmi wa huduma za kifedha kwa njia ya simu, tutahakikisha kwamba tunazingatia usalama, ufanisi na uhakika wa miamala ya wateja wetu.”
Mkuu wa Idara ya wa M-pesa Tanzania, Jacqueline Ikwabe, amebainisha umuhimu wa ushirikiano huu kwa kusema, “M-Pesa imejikita katika kuwezesha uvumbuzi wa kidijitali unaowanufaisha wafanyabiashara na wateja. Kwa kuiunganisha Bahati Nasibu ya Taifa kwenye jukwaa letu, tutahakikisha ushiriki salama, wa haraka na rahisi huku tukifungua fursa zaidi za ushirikiano katika sekta mbalimbali.”
Bahati Nasibu ya Taifa inalenga kutumia ushirikiano huu kuongeza uelewa wa huduma zake na kuimarisha uaminifu kabla ya uzinduzi rasmi wa Bahati nasibu ya Taifa. Hatua hii inatarajiwa kuweka msingi wa ushirikiano katika sekta ya michezo ya kubahatisha na fedha nchini Tanzania.
Ujumuishwaji wa jukwaa la Bahati nasibu ya Taifa kwenye majukwaa ya Vodacom Tanzania utarahisisha ununuzi wa tiketi na upatikanaji wa maudhui ya michezo ya kubahatisha kwa Watanzania wengi zaidi hapa nchini. Hatua hii ya kimkakati inatarajiwa kuongeza ushiriki wa umma, kupanua wigo wa huduma na kuhakikisha ushiriki mpana kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu.
MWISHO
Kuhusu ITHUBA
ITHUBA ni muendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa ya Tanzania, aliyeteuliwa kwa kipindi cha miaka nane kuanzia mwaka 2025. Kama sehemu ya kampuni inayoongoza katika uendeshaji wa bahati nasibu barani Afrika, ITHUBA inaleta utaalamu na ubunifu wa hali ya juu hapa Tanzania, kwa kuhakikisha uzoefu wa michezo ya kubahatisha wa viwango vya kimataifa. Kampuni imejizatiti kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha ajira, na kusaidia miradi ya michezo na jamii kwa ujumla.