Na John Walter -Hanang’
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameagiza Zahanati ya Kijiji cha Muungano, Kata ya Laghanga, kuanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo Aprili 30, 2025.
Agizo hilo limetolewa alipofanya ziara katika zahanati hiyo, ambayo ujenzi wake ulianza Septemba 2022 kwa nguvu za wananchi.
Hata hivyo, ujenzi huo bado haujakamilika kutokana na changamoto ya kifedha jambo ambalo mkuu wa mkoa ameonesha kutofurahishwa nalo na kutoa maelekezo hayo.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa wananchi wametimiza wajibu wao kwa kuanzisha mradi huo, hivyo hawapaswi kusumbuliwa tena.
Ameelekeza Halmashauri kuhakikisha ujenzi unakamilika ili wananchi waanze kufaidika na huduma za afya.
Aidha, amethibitisha kuwa Aprili 30, 2025, atarejea kuizindua rasmi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Geoffrey Abayo, ameahidi kuwa kufikia tarehe hiyo, ujenzi wa zahanati utakuwa umekamilika na tayari kwa kutoa huduma.
Eliwaza Qwari, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Muungano, amesema kijiji kilipokea shilingi milioni 91 kwa ajili ya mradi huo, lakini umekumbwa na ucheleweshaji kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.
Mbunge wa Vijana Taifa, Asia Halamga, amepongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa kwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa ukaribu, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kweli ya kuboresha huduma za jamii.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza azma yake ya kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika kwa wakati, akitumia kauli mbiu yake: “Hatuvui buti mpaka kieleweke.”