Na Seif Mangwangi, Arusha
WAKATI kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid ikiwa imeshafikia watanzania Milioni 43, wakazi wa Arusha wametakiwa kuwasilisha kero na migogoro ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu kwenye jopo la wanasheria kupitia kampeni hiyo waliofika Arusha tayari kuanza utatuzi wa migogoro kwa siku 10 mfululizo.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo ya msaada wa kisheria Mkoa wa Arusha ya Mama Samia Legal Aid, leo Machi 28, 2025 Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema ujio wa wanasheria hao ni upendeleo wa hali ya juu kwa wakazi wa Arusha na upendeleo wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wakazi wa Arusha.
Amesema kampeni hiyo ambayo ilishafanyika wiki ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani iliyofanyika kuanzia Machi 1 hadi 8, 2025 jijini Arusha iliweza kutatua migogoro mingi lakini haikuweza kumalizika hivyo aliwasilisha ombi maalum Serikalini na sasa wamerejea tena.
“Nawaomba wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kuleta kero na migogoro yenu kwenye timu hii ya wanasheria, wewe hata kama huna mgogoro wowote unaweza kufika na kujifunza hata mambo ya mirathi na wewe siku likikukuta unachukua hatua,”amesema.
Makonda ameagiza Halmashauri ya Arusha, Wilayani Arumeru kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na barabara ya Mianzini – Timbolo ambao mahakama imeshapitisha hukumu na kuwapa ushindi na kwamba hata mwanasheria mkuu ameshasema walipwe kwa kuwa hawezi kuingilia mamlaka ya mahakama.
“kwa kuwa Mwanasheria Mkuu ameshasema walipwe sidhani kama kuna ambaye ataweza kupindisha hivyo nawaomba wananchi wangu hata msipange foleni hapa nendeni jambo lenu limeshapata ufumbuzi, kama hamtalipwa tatizo litakuwa kwa mkurugenzi na hapo tutajua tatizo liko wapi na yeye najua anaipenda kazi yake sidhani kama anaweza kuacha kulipa,”amesema.
Awali akitolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi hao alipokuwa akitoa salamu za ofisi yake mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema ofisi yake ilishapokea malalamiko ya wananchi wa Mianzini kuhusu kulipwa fidia na yanafanyiwa kazi kwa kuwa tayari mahakama ilishatolea hukumu na kuwapa wananchi ushindi.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri wa sheria na katiba, Damas Ndumbaro amesema Arusha ni Mkoa wa 23 kufikiwa na kampeni hiyo ambapo tayari mikoa 22 imeshatembelewa na kero mbalimbali zimetatuliwa na wanasheria kupitia kampeni hiyo ya samia Legal Aid.
“Katika mikoa 22 ambayo imeshafikiwa na wanasheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid, jumla ya watanzania milioni 2192372 wametatuliwa migogoro yao kati yao wanaume wakiwa Mil 188457 na wanawake ni 1103915 na kupitia vyombo vya habari zaidi ya watanzania Mil 43 wamefikiwa,”amesema.
Aidha Waziri Ndumbaro amesema baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo wizara imekuja na mpango maalum wa kuanzisha madawati ya kisheria katika kila halmashauri ambapo maafisa maendeleo ya jamii watakuwa wakisikiliza migogoro na kuipatia utatuzi.
“ Pia tumeingia makubaliano na chama cha wanasheria Tanganyika ambao sasa wataendelea kutoa msaada wa kisheria kupitia wanasheria wao waliotawanyika kote nchini, tumeshawapatia mafunzo wanasheria 216 hapa Arusha na kwa nchi nzima wanasheria 22005 wamepatiwa mafunzo, lakini pia tumeingia mkataba na chuo kikuu huria ambao na wenyewe watakuwa wakisikiliza migogoro na kutoa msaada wa kisheria,”amesema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, kampeni hiyo Mko wa Arusha itafanyika kwa siku 10 kuanzia leo Machi 28, 2025 ambapo wanasheria hao watakuwepo katika wilaya zote za Mkoa wa Arusha kwaajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuipatia suluhu.