Na Seif Mangwangi, Arusha
MAOFISA wa Serikali watakaobainika kuhusika kuchochea migogoro mbalimbali dhidi ya wananchi na kupelekea kuichukia Serikali wanatarajiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kukomesha tabia hiyo dhalimu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda akizungumza leo Machi 27, 2025 katika ufunguzi wa semina ya timu itakayoshughulikia migogoro Mkoa wa Arusha kupitia kampeni ya kisheria ya “Samia Legal Aid Campaign” ameiagiza timu hiyo ya watoa huduma kuorodhesha majina ya watumishi wa serikali katika sekta mbalimbali watakaobainika kutajwa na wananchi kuwa wanachochea migogoro inayopelekea wananchi kuichukia Serikali.
Makonda amesema kuna baadhi ya maofisa maendeleo ya jamii wanalalamikiwa kwa kupindisha sheria ikiwemo watumishi wengine hivyo katika kampeni hiyo endapo kuna watumishi atakuwa analalamikiwa kukwamisha utatuzi wa migogoro kwa wananchi wakuu wa timu husika kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waandike majina yao kisha mwisho wa kampeni hiyo watoe taarifa kwake ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Kuna baadhi ya watumishi wanatajwa na wananchi kutokana na tabia ya kukwamisha mambo tunaomba majina yao, lakini pia naomba timu hizi zianishe changamoto zote zilizoibuka ili kupelekwa mahali husika kama polisi, uhamiaji, idara ya kazi na kwingineko ili hatua stahiki zichukuliwe “
Hata hivyo, amewasihi watoa huduma hiyo kuhakikisha wanawasilikiliza wananchi wanaofika kupata msaada huo ikiwemo watoa huduma hao kujiuliza nafsini kwao je maamuzi watakayotoa ni sahihi na hakuna upendeleo ili wahusika wapate haki yao kwa mujibu wa changamoto
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Ester Msambazi amesema kampeni hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2023 huku Mkoa wa Arusha ukiwa ni wa 23 tangu kampeni hiyo kuanza na wamejipanga vema kuanza kutoa msaada huo.
Uzinduzi wa kampeni hiyo utafanyika Machi 28, 2025 kwenye viwanja vya Ngarenaro ambapo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk, Damas Ndumbaro na Mkuu wa Mkoa Paul Makonda watahudhuria huku huduma na elimu za kisheria zikitolewa.
Huduma zingine zitakazotolewa ni utoaji wa huduma za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi pamoja na idara na ofisi mbalimbali za serikali na baada ya hapo timu husika zinaenda uwanjani kuanza kazi rasmi Machi 29,mwaka huu.
Mawakili, maofisa maendeleo ya jamii pamoja na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali wamehudhuria semina hiyo kwaaajili ya kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto za wananchi katika halmashauri saba za Mkoa wa Arusha pamoja na kuainisha changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kila idara husika.