Na Mwandishi Maalum,Mbinga.
WAKAZI zaidi ya 60,868 wa kata nane katika Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wanat
arajia kuondokana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama baada ya Serikali kutenga Sh.bilioni 4,010,608,417.63 ili kuboresha huduma ya maji katika kata hizo.
Kati ya fedha hizo Sh.milioni 755,194,120.25 ni gharama za Mkandarasi Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd itakayojenga mradi huo na Sh.bilioni 3,255,414,297.38 gharama za kutengeneza na kusafirisha mabomba ya kusambaza maji kutoka kiwandani hadi Wilaya ya Mbinga kazi itakayofanywa na Kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd.
Hayo yamesema jana na Mkurgenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga Mjini(Mbiuwasa) Mhandisi Yonas Ndomba,wakati wa hafla fupi ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji huo.
Alisema,mradi huo utahusisha ujenzi wa vyanzo viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 1,613,200,kujenga matenki manne ya ujazo wa lita 525,000,kujenga mtandao wa bomba wenye jumla ya kilometa 57.
Ndomba amezitaja kazi zinazokwenda kunufaika ni Ruhuwiko,Mbinga A,Betherehem,Matarawe,Lusonga,Masumuni,Mbinga Mjini B na Mbambi.
na mradi utakapokamilika huduma ya maji katika kata hizo nane itapatikana kwa asilimia 97.8.
Aidha alisema,kwa sasa mahitaji ya maji kwa siku ni lita 5,478,000 na uzalishaji kwa siku ni wastani wa lita 3,797,000 sawa na asilimia 69, hivyo kuwa na upungufu wa lita 1,681,000 hali inayopelekea huduma ya maji kutolewa kwa mgao katika Mji wa Mbinga.
Ndomba,ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya maji kwa kutenga fedha na kutoa kibali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo utakaohudumia wakazi wa Mbinga Mji.
Akizungumza na watumishi wa Mbiuwasa,viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi waliofika kushuhudia zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori alisema,kupitia mradi huo Mbiuwasa itakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita 1,681,000 ambazo ni pungufu kwa sasa.
Makori,amezitaka kampuni hizo kuzingatia muda na viwango katika utengenezaji wa mabomba na utekelezaji wa mradi na kuhakikisha mradi unawanufaisha wananchi wanaozunguka eneo la mradi kwa kutoa ajira za muda.
Ameongeza kuwa,malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ni kufikisha asilimia 95 maeneo ya mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu,lakini kupitia mradi huo Mji wa Mbinga utafikisha asilimia 98.3 hivyo kuvuka lengo.
Makori,amemtaka Mkandarasi Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd mara itakapoanza kazi kuhakikisha inalipa fedha za vibarua kwa wakati ili kuepusha malalamiko na migogoro inayoweza kuchelewesha kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mbiuwasa Mhandisi Patrick Ndunguru,amewaagiza watendaji wa Mbiuwasa kumsimamia kwa karibu Mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka na wananchi kushiriki kwenye kutunza vyanzo vya maji na miradi inayotekelezwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Mkazi wa kata ya Masumuni Mbinga mjini Moses Mapunda,ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji huduma ya maji ambayo kwa sasa inatolewa kwa mgao.
Alisema,kupatikana kwa mradi huo kutatoa majawabu ya kero ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu kwa wananchi wa kata nane na wakazi wa maeneo mengine katika Mji wa Mbinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma(Mbiuwasa)na Mhandisi Yonas Ndomba kushoto na mwakilishi wa kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd Elias Nyenzi,wakionyesha mikataba ambapo kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd imepata kazi ya kutengeneza na kusambaza mabomba ya maji kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji katika mji wa Mbinga.