Na. Josephine Majura, WF, Buchosa, Mwanza
Serikali imezitaka Taasisi za Fedha nchini kutoa elimu kwa wakopaji ili wawe na uelewa mpana kuhusu masharti ya mikopo, viwango vya riba, gharama za ziada, na athari za kutorejesha mkopo kwa wakati kabla ya kusaini mikataba husika.
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake kwa wananchi wa Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Alifafanua kuwa Taasisi za Fedha zinapaswa kutoa taarifa sahihi na mafunzo kwa wateja wao kabla ya kusaini mikataba ya mikopo ili kuhakikisha wanachukua uamuzi wa kukopa wakiwa na taarifa sahihi.
“Serikali inaendelea kuweka sera na miongozo inayolinda wakopaji dhidi ya unyonyaji wa kifedha na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa maendeleo ya kiuchumi”, alisema Bw. Myonga.
Aliongeza kuwa kukiwa na uwazi katika utoaji mikopo na elimu ikatolewa vizuri kwa wakopaji kutapunguza unyonyaji wa kifedha na kutawasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kwenye mikopo wanayoomba.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Bi. Grace Machunda, aliwahamasisha wanavikundi mbalimbali nchini kusajili vikundi vyao ili kupata mikopo ya Serikali na kusaidiwa kisheria kutakapotokea changamoto kwenye vikundi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, mkazi wa Buchosa, Bw. Musa Kilaba, aliwashauri washiriki wenzake wa mafunzo hayo kwenda kufanyia kazi walichofundishwa.
Bw. Kilaba aliishauri Serikali kuongeza semina za mafunzo ya elimu hiyo katika ngazi zote nchini na kuongeza idadi wa watoa elimu ili waweze kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja.
Naye Bi. Laurencia Msabi, mkazi wa Buchosa, aliahidi kuwa Balozi wa elimu ya fedha katika vikundi ambavyo ni mwanachama na jamii inayomzunguka.
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalilimbali ikiwemo mikopo, akiba na uwekezaji zilizofundishwa wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Buchosa, Mwanza)