Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) katika Halmashauri mbalimbali hapa Nchini wametakiwa kuhakikisha wanahakiki majina ya walengwa pamoja na namba zao za simu wanazotumia kupokea fedha za Mpango wa Kaya Maskini ili kuepusha fedha hizo kwenda sehemu nyingine.
Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi Taifa ya TASAF Peter Ilomo ameyabainisha hayo wakati wa hitimisho la ziara yake Wilayani Chemba ambapo ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF katika halmashauri za mkoa wa Dodoma na wilaya zake, ikiwemo miradi ya maji, elimu na afya.
Amesema ni vema waratibu wakalifanya zoezi la uhakiki mapema ili kujiridhisha kama walengwa wameandika namba sahihi za simu, pamoja na majina sahihi ya mlengwa anayestahili kupokea fedha hizo kwa ajili ya kujikimu wao na familia zao.
“Naomba waratibu fuatilieni suala la uhakiki wa majina pamoja na namba za simu ili kuwa na uhakika na walengwa wenu kuwa wote wanapokea fedha za Mpango wa Kaya Maskini kwa wakati”, alisema Ilomo.
Amesema lengo lao ni kuona kila mlengwa wa TASAF anapokea fedha hizo kwa wakati ili aweze kujikwamua yeye na familia yake ikiwemo kuzitumia kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo yeye na familia yake ili wajikwamue kiuchumi.
Hata hivyo amewapongeza walengwa wa TASAF kutokana na kupiga hatua za kimaendeleo kutokana na kuwekeza fedha wanazopewa na mfuko huo, kwa ajili ya kuanzisha biashara mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi.
Naye mlengwa Aziza Ally mkazi wa kijiji cha Gwandi kilichopo Wilayani Chemba aliishkuru serikali kupitia TASAF kutokana na kutoa fedha hizo kwa walengwa ambazo zimewasaidia kuwainua kiuchumi.
Amesema kabla ya kuingia katika mpango wa Kaya Maskini alikuwa na hali duni ya kimaisha, lakini hivi sasa amepiga hatua baada ya kuwekeza fedha hizo na kuanza kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinamwongezea kipato.
“Tunaishkuru sana serikali kutokana na kutoa fedha hizi kwa walengwa zinatusaidia sana kujikwamua kiuchumi na kusonga mbele”, alisema Aziza.
Akitoa shukrani kwa viongozi kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Gwandi Mathei Suki aliwaomba TASAF kuendelea kuleta miradi mingine ambayo itazidi kuwainua walengwa katika biashara ndogo ndogo wanazofanya.
Suki amesema kupitia fedha za TASAF walengwa wengi wameanzisha vikundi vya kukopeshana ambavyo vinawasaidia kujiongezea kipato wao na familia zao katika maeneo mbalimbali hapa nchini.