Wajasiriamali nchini wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazowazuia kufanikisha malengo yao, zikiwemo ukosefu wa mitaji, ujuzi wa biashara, nidhamu ya biashara, kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu soko, na changamoto za ubora wa bidhaa.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa AVODA Group, Jun Shiomitsu, wakati akieleza mkakati wa kampuni yake kuwainua na kuwawezesha wajasiriamali kupitia ubia wao na Unleashed Africa Social Enterprises.
Shiomitsu amesema kuwa licha ya wajasiriamali wengi nchini kuwa na biashara zenye mwelekeo mzuri, wanashindwa kuzikuza kutokana na ukosefu wa mbinu za ukuzaji wa biashara na uelewa mdogo wa masoko.
“Biashara zina changamoto nyingi sana, ili kuzikuza lazima wajasiriamali wajifunze mbinu bora za kuhudumia wateja, kutangaza bidhaa kwa ubunifu, na kushirikiana na wafanyabiashara wengine,” amesema Shiomitsu.