Na Mwandishi Wetu, Maswa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema nchi inakopa kwa ajili ya kufanya mambo tukayoishi nayo na faida zake zitakuwepo kwa miaka mingi kwa kizazi cha sasa na hata kijacho.
Amesema deni lililopo la Sh. trioni 97 sio kwamba lote limekopwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan bali limekuwepo tangu enzi za Rais wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wasira ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanachama pamoja na viongozi wa CCM Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu katika kikao cha ndani kikiwa sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi.
“Tunakopa ili kufanya jambo ambalo tutaishi nalo na faida zake kwa miaka mingi kizazi hiki na hata kizazi kijacho na lile deni sio kwamba amekopa Rais Samia trilioni 97 sio kweli, lile deni linaongezeka na madeni mengine ya zamani ambayo tulishakopa tangu enzi za Nyerere, alichukua miaka 40 kuanza kulipa nayo yamo katika hesabu,” amesema.