Na John Walter -Babati
Wananchi wa Tarafa ya Mbugwe, wilayani Babati, mkoani Manyara, wameeleza kilio chao mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, wakilalamikia wizi wa mifugo unaofanywa na watu wasiojulikana.
Wazee wa jamii ya kifugaji wamesema kuwa wizi huo umekithiri katika tarafa hiyo, hali inayowaathiri kiuchumi na kuleta hofu miongoni mwao.
Wakizungumza katika mkutano na Naibu Waziri, wameeleza kuwa mifugo yao imekuwa ikipotea mara kwa mara bila wahusika kukamatwa, jambo linalodhoofisha shughuli zao za ufugaji.
Kutokana na malalamiko hayo, Naibu Waziri Sillo ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea na msako wa wahusika wa matukio hayo.
Amehimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu kwa wakati ili hatua stahiki zichukuliwe mapema.
Tukio la wizi wa mifugo limekuwa tatizo kubwa kwa wakazi wa eneo hilo kwani mapema mwezi Machi 2025, wafugaji wa Tarafa ya Mbugwe waliandamana baada ya ng’ombe 14 kuibwa, ingawa baadaye 9 walipatikana.
Kutokana na hasira, wananchi walikusanyika wakiwa na fimbo na silaha za jadi katika mkutano uliofanyika Kijiji cha Matufa, Kata ya Magugu.
Kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata pamoja na Jeshi la Polisi, wananchi walitulizwa, na hatimaye polisi waliwakamata washukiwa wawili wanaohusishwa na matukio hayo ya wizi wa mifugo.
Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha ulinzi na usalama wa mali za wananchi, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya ulinzi katika kutokomeza uhalifu huo.