Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amewataka wadau na wafanyabiashara nchini kujitokeza na kuiga mfano wa kampuni ya huduma za kifedha, iTrust Finance Limited, kwa kudhamini jitihada mbalimbali za kibiashara, ikiwa ni pamoja na masoko ya bidhaa za wafanyabiashara wadogo na wa kati, hususani wanawake.
Waziri Jafo alitoa rai hiyo jana alipohudhuria maonesho makubwa ya Soko la Jiba Souk yaliyofanyika katika Viwanja vya Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wajasiriamali 250 walishiriki na kuvutia umati wa watu zaidi ya 13,000.
Katika mazungumzo yake, Waziri Jafo aliipongeza iTrust Finance kwa kushirikiana na wajasiriamali kama mdhamini mkuu wa tukio hilo muhimu, lenye lengo la kukuza fursa za biashara na uchumi miongoni mwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka iTrust Finance, udhamini huu ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kukuza uhuru wa kifedha, kwa kuunda fursa za maendeleo endelevu. Kampuni hiyo inalenga kusaidia biashara zinazofadhiliwa na wanawake, huku ikilenga kuimarisha uthabiti wa kifedha wa wajasiriamali hao kwa ajili ya siku zijazo.
“Fedha zetu za uwekezaji zitawasaidia wajasiriamali hawa kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya watoto wao, kuhakikisha mustakabali wao, na kufanikisha mpango wa kustaafu kwa amani,” ilisomeka taarifa kutoka iTrust Finance.
Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance, Faiz Arab, alisisitiza kuwa ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kufanikisha ujumuishaji wa kifedha kwa wamiliki wa biashara ndogo. Aliongeza kwamba kama kampuni inayojitolea kwa ujumuishaji na uwezeshaji wa kiuchumi, iTrust inaona udhamini huu kama njia ya kuziba pengo la kifedha na kuimarisha ustawi wa wafanyabiashara wadogo kwa muda mrefu.
“Juhudi hizi ni sehemu ya mpango wa iTrust W.I.S.E (Women in Investments and Securities Education), ambao unalenga kujenga jamii ya wanawake walioelimika kifedha na wenye nguvu katika kushiriki fursa za uwekezaji,” aliongeza Faiz.
Kampuni hiyo pia inawaalika wananchi kushiriki katika kusherehekea mafanikio ya wajasiriamali wanawake na kuonesha jinsi uwezeshaji wa kifedha unavyoweza kubadilisha maisha yao.
JIBA Dar es Salaam, ambayo ni mwenyeji wa Soko la Jiba Souk, ni sehemu ya JIBA International, shirika lililoanzishwa mwaka 1991 kwa lengo la kukuza fursa za biashara na uchumi miongoni mwa wanachama wake, hasa kutoka jamii ya kimataifa ya Khoja Shia Ithna-Asheri.