Mnamo tarehe 27 Machi 2025, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliungana na Ubalozi wa Uingereza pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa – Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme – WFP) katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni.
Uhamasishaji huu ulifanyika kupitia warsha maalum iliyowakutanisha walimu wakuu, wapishi, na walimu wa lishe kutoka shule 50 za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Katika warsha hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, aliambatana na Kaimu Meneja wa Utafutaji Rasilimali na Hamasa wa TEA, Dkt. George Mofulu.
Kwa upande mwingine, Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Marianne Young pamoja na Mwakilishi wa WFP nchini, Bw. Ronald Tran Ba Huy, walipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni na wakaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.