Wakala wa Vipimo Tanzania wamefanya ziara ya kushtukiza katika mabucha mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mizani, kuhakikisha vipimo vinazingatiwa ipasavyo, na kulinda haki za walaji.
Katika ziara hiyo, wakaguzi wa wakala wa vipimo walikagua mabucha yote kwa umakini, na hakuna mfanyabiashara yeyote aliyebainika kufanya ubadhilifu wa mizani. Mizani zote zilikuwa sahihi, jambo linaloashiria uelewa mzuri wa wafanyabiashara juu ya matumizi sahihi ya vipimo.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala amesema kuwa zoezi hili ni sehemu ya jukumu lao la kila siku kuhakikisha mizani inakaguliwa mara kwa mara ili kujiridhisha na usahihi wake. Alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuwalinda wananchi dhidi ya udanganyifu wa vipimo na kuhakikisha wanapata thamani halisi ya pesa wanazolipa.
Kwa upande wao, wauzaji wa nyama wamepongeza juhudi za wakala wa vipimo. Mack Zube, muuza nyama maarufu kutoka Segerea, ameishukuru serikali kwa ushirikiano wao mzuri na kwa kuwapa elimu ya matumizi bora ya mizani. Pia, amepongeza msimamo madhubuti wa wakala wa vipimo katika kuhakikisha sheria na kanuni za vipimo zinafuatwa ipasavyo.