Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema serikali inavuta mitaji kutoka sekta binafsi kwasababu kodi na mikopo hayatoshi kufikia matarajio ya wananchi.
Katika mazungumzo maalum na The Chanzo Machi 29,2025, Kafulila amesema deni la Tanzania ambalo ni Sh. trilioni 97 ni himilivu kwa uchumi wa Tanzania.
Amesema takwimu za Oktoba mwaka 2024 za IMF zilionesha kuwa deni la dunia limefika zaidi ya Dola Marekani trilioni 315 wakati uchumi wa dunia ukiwa Dola trilioni 110 ambako ni mara tatu ya uchumi wa duniani.
Aidha, amefafanua kuwa deni la dunia ndani yake kuna deni la sekta binafsi zaidi ya Dola trilioni 164, deni la kaya ambalo n idola trilioni 48 na deni la serikali trilioni 102 ambalo ni zaidi ya asilimia 90 ya uchumi.
“Kwa Afrika deni la serikali kwa uchumi ni takribani asilimia 67 kwa Tanzania ni takribani asilimia 47, deni linaongezeka ndio lakini ukifanya malinganisho kuna tofauti kubwa kati ya ukuaji wa deni letu kwa uchumi.
“Rwanda deni limefikia asilimia 71 ya uchumi, Kenya 70, Uganda 54, Malawi 84, Msumbiji 76 na Namibia 67,nchi nyingi zinakabiliwa na shida kubwa ya deni lakini sababu kubwa ni serikali kutaka kukidhi matarajio ya watu kwa kuwapa huduma za maji, umeme, afya na barabara.”