Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
JAJI wa Mahakama Kuu Dodoma Amiri Mruma amelishauri Baraza la Masoko ya Mitaji kuhakikisha kuwa linajisimamia kwa uhuru katika utendaji wake ili wananchi waweze kupata haki na kuwekeza zaidi.
Ameongeza kwamba kuwa ili uchumi wa taifa ukue, ni lazima wawekezaji wahakikishiwe kuwa haki zao zinalindwa, hivyo baraza linapaswa kuwa huru bila upendeleo kwa mtu yeyote au taasisi yoyote.
Ametoa ushauri huo leo Aprili 2,2025 jijini Dar es Salaam katika ya kumuaga Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Baraza la Masoko ya Mitaji Dk.Deo Nangale ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa na kukabidhi kijiti kwa Mwenyekiti mpya wa baraza hilo Dk.Ntemi Kilekamajenga.
Jaji Mruma amesema ni vema baraza hilo likawa huru katika kutekeleza majukumu na kuongeza katika utoaji wa haki, upendeleo hauna nafasi.
“Hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu bila woga au upendeleo ili mpate tena uteuzi.Wananchi wanahitaji haki ili wawe na imani kubwa zaidi katika masoko ya mitaji vilevile, utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya baraza hili ni jambo la msingi.
“Kuna mabaraza mengi yanayofanya kazi vizuri nchini,mfano Baraza la Ushindani, ambalo limekuwa likishughulikia kesi nyingi za aina mbalimbali na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao,”amefafanua Jaji Mruma aliyekuwa akitoa uzoefu wake kwa Mwenyekiti mpya wa baraza hilo pamoja na maofisa wengine.
Kwa upande wake, mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dkt Deo Nangela, ametumia nafasi hiyo kueleza umuhimu wa baraza kuendelea kujitangaza ili wananchi waweze kulitambua na kupata fursa ya kueleza changamoto zao alionya kuwa bila hilo, baraza litapoteza umuhimu wake.
Ameongeza kwamba kuna wananchi wengi wanaopitia changamoto mbalimbali katika masoko ya mitaji, lakini hawajui wapi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao. Hivyo, uwepo wa baraza hilo ni muhimu kwa kuwa linasaidia kutatua matatizo yao,” alisema.
Amefafanua katika kipindi kifupi alichohudumu kama mwenyekiti, kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, mafunzo mbalimbali yalifanyika, yakiwemo yale ya kujifunza kutoka kwa nchi jirani kama Kenya ili kupata uzoefu zaidi.
Wakati huo huo Mwenyekiti mpya wa baraza la Masoko ya Mitaji Jaji Dkt Ntemi Kilekamajenga ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na mtangulizi wake ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu baraza na kwamba mashauri yataanza kusikilizwa kwa wakati ili kutatua changamoto za wawekezaji.
Amesema baraza hilo ni muhimu kwa sababu mara nyingine mahakama hushughulikia kesi ambazo kimsingi zinapaswa kushughulikiwa na wataalamu wa masoko ya mitaji. Hivyo, wataendelea kutoa elimu na mafunzo mbalimbali ili baraza lijulikane zaidi kwa wadau.
Awali Msajili wa Baraza, Martini Kolikoli, amesema kuwa baraza hilo lina jukumu la kuhakikisha kuwa sekta ya masoko ya mitaji inaendelea kuwa na mazingira rafiki kwa wawekezaji.
Pia amesema baraza linajivunia kuwa sehemu ya juhudi za kitaifa za kufanikisha malengo yaliyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambapo masoko ya mitaji yanatambuliwa kama nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuimarisha uwekezaji wa muda mrefu.
Aidha, katika utekelezaji wa nafasi yetu kisheria, wanaendelea kutoa shukrani za dhati kwa wadau wetu wote, hususan Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwa kuendelea kushirikiana nasi na kuhakikisha kuwa sekta hii inaendelea kukua na kuwa jumuishi kwa wawekezaji na wadau wote.
“Ni matumaini yetu kuwa chini ya ongozi wa Dkt. Ntemi Kilekamajenga, Baraza litaendelea kuwa nguzo imara katika kuhakikisha haki inatendeka kwenye sekta ya masoko ya mitaji na dhamana kwa mujibu wa sheria, na hivyo kuzidi kuimarisha imani ya wawekezaji na wadau wote katika soko letu.”