Na Seif Mangwangi,Arusha
KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid imebaini uwepo wa migogoro mingi ya Ardhi katika Halmashauri ya Meru Wilayani Arumeru inasababishwa na Ndugu kudhulumiana mali za urithi ikiwemo ardhi.
Migogoro hiyo imebainika kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la uzinduzi wa kampeni ya Samia Legal Aid katika eneo la Malula katika kata ya King’ori, Halmashauri ya Meru, Wilayani Arumeru leo Machi 31, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Sheria na Katiba, Damas Ndumbaro, aliyekuwa mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa amesema migogoro hiyo imekuwa ikisababishwa na ukosefu wa kutoandikwa kwa mirathi.
” Ukiona mwananchi amekuja hapa Meru ujue ni mgogoro wa ndugu kwa ndugu kudhulumiana ardhi ambazo zinatokana na mirathi, na wanaodhulumiwa hasa ni wanawake, ” amesema Mkalipa.
Amesema ili kuepuka migogoro ya aina hiyo, wananchi wa Meru wanatakiwa kujifunza umuhimu wa kuandika wosia pindi wakiwa hai na kuwataka wanaoachiwa mirathi hiyo kuitii.
“Kwa kuwa huku kwenu imebainika migogoro mingi inatokana na dhuluma ya mali hasa ardhi, leo mtapewa elimu ya mirathi na namna ya kuandika wosia, tunataka hii migogoro iishe kabisa, lakini pia mtapewa elimu ya ndoa,”amesema.
Wakiwasilisha migogoro yao mbele ya Mkuu wa Wilaya wananchi wa kijiji cha Malula wamelalamikia kutaka kupokonywa mashamba ambayo wamekuwa wakiyalima tangu mwaka 1972.
Wananchi hao wamemtaja mwananchi mmoja kwa jina la Zara kuwakataza kulima mashamba hayo akidai yeye ndio mmiliki wa mashamba hayo tangu miaka ya 1960 akiyarithi kutoka kwa marehemu wazazj wake.
Mkuu wa Wilaya Amir Mkalipa aliwaeleza wananchi hao kuwa mgogoro huo anaufahamu vizuri na kwamba mashamba hayo ni mali ya Serikali na imeshayatenga kwaajili ya eneo la uwekezaji (EPZ), na kwamba hakuna mtu yoyote aliyemilikishwa.
” Mashamba ya malula ni eneo la Serikali, yameshatengwa kwaajili ya uwekezaji wa EPZ lakini kama Serikali tutakuja kuwasikiliza na tutawapanga kwa muda ili muendelee kuyalima lakini sio kuwamiliķisha na watu wachache waliojenga nyumba zao zinaenda kubomolewa,”Amesema DC Mkalipa.
Mkurugenzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid, Wakili Ester Msambazi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe msaada wa kisheria kwa kuwa huu ndio muda sahihi.
“Ikitokea uko eneo la jirani jitokeze ili utatuliwe tatizo lako kwa kuwa ndio sehemu sahihi kwa sasa ili uweze kupata msaada, tuna mawakili wenye ubobezi wa Mambo mengi kama ardhi, ndoa, mirathi, kazi,” amesema Wakili Ester.