Na Pamela Mollel,Arusha
Zaidi yawafanyabiashara na wajasiriamali 100 kutoka nchini wanatarajia kuhudhuria jukwaa maalumu la kimataifa linalohusu maswala ya uwekezaji nchini Israel kwa ajili kubadilishana uzoefu na fursa za miradi ya uwekezaji zinazoweza kutekezwa na wataalamu hao katoka nchi hizo mbili.
Wafanyabiashara hao wanatarajia kukutana katika mji wa Tel-aviv nchini Israel june 8 hadi 14, 2025 katika jukwaa la Biashara na Uwekezaji ya Tanzania-Israel (TIBIF) .
Lengo kubwa katika jukwaa hilo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Israel, kukuza ushirikiano na ubunifu lakini pia kubadilishana fursa za uwekezaji na miradi inayoweza kutekelezwa na nchi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) Isaac Mpatwa amesema kuwa wameandaa safari hiyo kwa ajili ya kuwapa fursa wajasiriamali na wafanyabiashara kukutana, kujitambulisha, na kuchunguza ushirikiano unaowezekana na wenzao wa Israel katika Nyanja mbalimbali.
“Tunawapeleka wafanyakabiashara wetu nchini Israel ili kuwaunganisha na masoko, miradi, mitaji, fedha, mafunzo, na ushauri wa kibiashara katika sekta mbalimbali za uwekezaji wa elimu, ufugaji, uvuvi, viwanda, teknolojia na utalii” amesema na kuongeza
“Tunataka wafanyabiashara wetu wapate nafasi ya kukutana na wenzao wa Israel kupitia mikutano midogo midogo ya kibiashara ‘Business to Business Meeting[B2B]’ iliwaweze kufaidika na fursa za biashara zinazofanana na wenzao”
Mpatwa amesema kuwa hayo yote yanafanyika kwa ushirikiano na serikali chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji, na Wizara ya Mambo ya Nje.
“Ushirikiano huu unalenga kubadilishana maarifa, miradi, na uzoefu kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanaungwa mkono na mifumo rasmi ya kiuchumi na unatoa fursa za kufanikisha makubaliano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na serikali, au serikali za nchi washirika na nchi yetu”.
Mpatwa ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mtandao wa kuwaunganisha wafanyabiashara na wajasiriamali na fursa mbalimbali za kiuchumi ndani na nje ya nchi iliyopewa jina la ‘KLI Alumni Connect’.
Mtandao huo utawahusisha wafanyabiashara waliopitia programu za uongozi wa Biashara na ujasiriamali katika kipindi cha miaka mitatu kilichoendeshwa na KLNT kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Regent kilichoko nchini Marekani.
Mpatwa amesema mtandao huo utakaowakutanisha wahitimu wa elimu ya vitendo ya biashara na ujasiriamlali kutoka kituo cha kibiashara cha Business Development center (BDC) Tanzania unalenga kuwawezesha kukuza na kuimarisha biashara zao walizonazo.
“Kupitia KLI Alumni Connect, tunawapa wahitimu wetu fursa ya uunganishwa na ekosistemu ya biashara, mabenki, taasisi za maendeleo ya teknolojia, na wadau wa ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya mataifa 100 duniani tulizo na mahusiano nazo”.
Amesema hiyo itawawezesha kupata Elimu zaidi, mitaji, ubunifu, teknolojia, vifaa, na masoko ya kimataifa.
Mmoja wa wafanyabiashara wahitimu katika programme hiyo, Rephrine Kombe amesema mafunzo hayo ya wiki 20 yamewasaidia kuwapa ujasiri wa kuwasilisha mawazo yao na kuboreshwa na wataalamu hao wa biashara na kuwasaidia kuanza safari rasmi ya kibiashara.
“Mimi nilikuwa na wazo tayari, hivyo nikasaidiwa kuboresha na wakufunzi wetu ambao ni maprofesa wa biashara, na sasa nimefanikiwa kuwa na biashara halisi, na zaidi nimefanikiwa kuingia kwenye mfumo rasmi wa kiserikali” amesema Rephrine ambae ni Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza taulo za kike cha Reepads’ .
Aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Programe hiyo, Meya wa jiji la Arusha Maximmilian Iranghe amesema kuwa elimu hiyo ya ujasiriamali ya vitendo ni nzuri ambayo inasaidia pia serikali kukuza ajira na kukua kiuchumi kwa jamii.
“Kadri wananchi wake wanavyokua na uchumi mzuri ndivyo na serikali inavyozidi kukua hivyo niwapongeze sana KLNT na niseme kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara na wajasiriamali wote nchini hasa katika kutatua changamoto zao wanazokumbana nazo ili kukuza biashara zao”.
Pia amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanatumia fursa ya uwekezaji wa nyumba za wageni ili kuchangamkia fursa ya utalii inayozidi kukua kila kukicha huku changamoto kubwa ikiwa malazi.
“Tena uwekezaji huo muanze sasa hivi maana mwaka 2027 kuna utalii mkubwa wa mikutano na wa michezo ambazo tutakuwa na mkutano mkubwa wa wadau na wataalamu wa nyuki duniani watakaokutana Arusha unaojulikana kama ‘Apimondia’ lakini pia michuano ya kombe la Afrika ‘Afcon’ hivyo changamkeni hela zinakuja” amesema Meya huyo.