Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya Sh. Trilioni 7.53 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ufanisi wa asilimia 101.32 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 7.43.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda imeeleza kuwa ufanisi wa makusanyo ya Robo ya Tatu ya mwaka 2024/2025 ni sawa na ukuaji wa asilimia 13.47 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 6.63 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa makusanyo yaliyokusanywa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25 yanapelekea TRA kuweza kuweka rekodi ya kipekee katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 9 mfululizo katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa ya Bw. Mwenda inafafanua kuwa katika kipindi cha mwezi Julai – Machi, mwaka wa fedha 2024/25, TRA imekusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 24.05 sawa na ufanisi wa asilimia 103.62% ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 23.21, na ukuaji wa asilimia 17.01 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 20.55.
Aidha, makusanyo hayo ni ya kiwango cha juu kabisa kufikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kipindi kama hicho toka kuanzishwa kwake, na ni sawa na ongezeko la asilimia 77 toka kiasi cha Shilingi Trioni 13.59 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2020/21, miaka minne toka Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aingie madarakani.
Ufanisi huu katika makusanyo uliofikiwa mwezi Julai – Machi mwaka wa fedha 2024/25 ni matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanayohusiana na uongezaji wa uhiari wa ulipaji kodi kupitia uboreshaji wa huduma kwa walipakodi na uboreshwaji wa shughuli za biashara nchini.
Katika taarifa hiyo Bw. Mwenda anataja hatua zilizochukuliwa na kufanikisha ufanisi huo wa makusanyo kuwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais la kuhamasisha ulipaji Kodi wa Hiari nchini.
Hatua nyingine amesema ni kuongezeka kwa utendaji kazi mzuri, nidhamu na ubunifu kazini kwa watumishi wote wa TRA kwa kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na Jumuiya za wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wote nchini na Kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa njia mbalimbali kwa wafanyabiashara wote nchini.
Pia kuanza matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa, uliozinduliwa mwezi Januari 2025, ili kuimarisha usimamizi wa vyanzo vyote vya mapato vya Forodha na Kufuatilia kwa ukaribu hali ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu uzalishaji wa viwandani na matumizi mashine za kielektroniki (EFD) nchini.
Hatua nyingine ni kuendelea kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma bora zinazozingatia mahitaji ya walipakodi, kuwahudumia walipakodi siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) kupitia ofisi zote za TRA nchini na
kuendelea kuboresha mahusiano na wafanyabiashara na kutatua changamoto za biashara kwa kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa ni siku maalum ya ‘Kusikiliza Walipakodi’ kupitia ofisi zote za TRA nchini.
Hatua nyingine ni kuendelea kutekeleza mikakati na kampeni za uhamasishaji wa uhiari wa ulipaji kodi nchini na Serikali kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini, hali iliyopelekea Kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayoingizwa au kuondoshwa nchini.
Pia Kuendelea kuongeza mahusiano baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na wawekezaji kupitia njia za majadiliano na mikutano na Kuendelea kuongezeka kwa idadi ya Waendesha Uchumi Walioidhinishwa (Authorized Economic Operators) nchini.
Bw. Mwenda katika taarifa yake anaeleza mikakati iliyowekwa na Menejimenti ya TRA ili kuhakikisha miezi iliyosalia kukamilisha mwaka wa fedha 2024/2025 wanavuka malengo ya makusanyo kuwa ni Kutekeleza maagizo yote ya Mhe. Rais.
Kukamilisha ujenzi wa moduli zote za Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ifikapo Juni 2025, Kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na walipakodi kupitia utoaji wa huduma bora pamoja na kampeni za elimu kwa mlipakodi.
Pia kuendelea kuimarisha usimamizi wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD nchini kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji, pamoja na kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD kwenye maendeleo ya nchi.
Aidha Bw. Mwenda ametaja mkakati mwingine kuwa ni Kuendelea kusimamia na kuimarisha misingi ya mfumo mzuri wa kodi, ikiwemo Haki na Usawa katika utozaji kodi (no favouritism or victimization) ili kuweka mazingira ya biashara yaliyo sawa na Kushirikiana kwa kikamilifu na timu iliyoteuliwa na Mheshimiwa Rais inayofanya mapitio ya mfumo wa utozaji kodi nchini ili kuleta maboresho.
Kuimarisha na kusimamia weledi (professionalism) na huduma nzuri kwa walipakodi (customer service) ikiwemo watumishi wetu wote kuvaa vitambulisho muda wote wanapotoa huduma.
Pia TRA itaendelea Kuimarisha vitengo vya Ukaguzi na Uchunguzi wa Kodi ili Kuzuia ukwepaji kodi za ndani na Forodha na kuondoa upotevu wa mapato ya Serikali ili kuweka mazinigira ya biashara yaliyo sawa kwa wafanyabiashara wote.
Bw. Mwenda katika taarifa yake amewashukuru Walipakodi kwa kuendelea kulipa Kodi kwa hiari na kuiamini TRA.