
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Geita, Gabriel Nyasilu, amesema kuwa uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa CCM kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 umetokana na rekodi yake ya mafanikio, hasa katika kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa na Hayati Dkt. John Magufuli.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya UWT Tawi la Msalala Road, Nyasilu alitaja Mradi wa Daraja la Magufuli – linalojengwa katika Kanda ya Ziwa – kama mfano hai wa miradi inayotekelezwa kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Utekelezaji wa miradi kama Daraja la Magufuli unaonyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia kuendeleza maendeleo ya kweli kwa wananchi,” alisema Nyasilu.
Daraja hilo linatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha usafiri na biashara, likirahisisha mawasiliano kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuleta fursa mpya kwa jamii zinazolizunguka.