Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
VIONGOZI wastaafu Afrika pamoja na wataalamu wa maendeleo wametoa mwito kwa Serikali barani humo kutekeleza mikakati inayotambua na kutoa motisha kwa watu wanaowekeza katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Mwito huo umetolewa Machi 8,2025 katika Jiji la Kampala nchini Uganda katika siku ya pili ya Mkutano wa 8 wa Viongozi wa Afrika (ALF), unaoendelea chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi – Uongozi Institute.
Mlezi wa Kongamano hilo na Rais wa Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kuwawezesha wananchi wao, hususan wataalamu wa majadiliano wa masuala ya mazingira, ili waweze kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa.
“Tunaponyimwa fursa ya kutumia ipasavyo rasilimali zetu na badala yake zikanufaisha mataifa yenye nguvu kiuchumi, tunajikuta tukikosa uwezo wa kushughulikia changamoto kama mabadiliko ya tabia nchi na uhifadhi wa misitu,” amesema Rais mstaafu Kikwete.
Ameongeza, “Tunatoa motisha kwa watu wanaopanda miti mipya, lakini hatuwatambui wala kuwathamini wale wanaolinda misitu iliyopo. Hii inaleta pengo kubwa katika juhudi za uhifadhi na kudhoofisha azma ya kulinda ikolojia ya asili.”
Amesisitiza kuwa mfumo wa sasa ambao unamnufaisha kifedha mharibifu wa mazingira huku mhifadhi akikosa chochote, hauwezi kudumu. “Ni lazima tubadilishe mtazamo huu kwa kutambua mchango wa misitu katika kuhifadhi kaboni…
“Na kuwazawadia wanaojitolea kuilinda,” amesema na kufafanua uwepo wa fursa ya makubaliano kati ya serikali na wadau yatakayohusisha malipo kwa ajili ya ulinzi wa misitu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia na Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo, Hailemariam Desalegn Boshe, amesema
kuwa uhaba wa fedha za tabia nchi ni kikwazo kikubwa kwa Afrika kunufaika ipasavyo na fursa za uhifadhi wa mazingira.
“Ni muhimu tuwe na mshikamano na tushirikiane kama bara katika majadiliano ya kimataifa ili kuhakikisha tunapata manufaa halisi kutoka kwenye biashara ya uhifadhi wa misitu,” amesema Boshe.
Hata hivyo amehimiza nchi za Afrika kuunda timu thabiti za wajadiliano zitakazotetea kwa nguvu maslahi ya bara katika mikutano ya kimataifa kuhusu mazingira.
Wakati huo huo Dkt. David Obura, ambaye ni Mkurugenzi Mwanzilishi wa shirika la CORDIO Afrika Mashariki, alizungumzia umuhimu wa maboresho katika sheria za tabianchi ili kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uhifadhi wa misitu.
“Kwa sasa tunahitaji kujenga mifumo imara ya fedha za tabianchi itakayovutia uwekezaji katika sekta ya mazingira, hasa uhifadhi wa misitu,” alisema Dkt. Obura.
Kwa upande wake. Profesa Chukwumerije Okereke ambaye ni Mtaalamu wa utawala wa tabianchi na sera za umma kutoka Chuo Kikuu cha Bristol, aliwasilisha mapendekezo matano muhimu:
Mapendekezo hayo ni kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za tabianchi, kuwekeza kwenye maeneo yenye thamani kubwa ya kiuchumi, kutumia suluhisho za ndani, kusisitiza haki ya tabianchi, na kuifafanua upya dhana hiyo ili iwe na muktadha wa Kiafrika.
Profesa Okereke amebainisha kuwa licha ya hatua zilizopigwa, bara la Afrika bado linakabiliwa na pengo la kifedha linalokadiriwa kuwa dola bilioni 2.8, linalozuia juhudi za uendelezaji wa uhifadhi wa mazingira.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu Afrika: Njia ya Mbele,” umewakutanisha wataalamu wa maendeleo, watunga sera, wadau wa mazingira, na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.
Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ndiye aliyefungua rasmi mkutano huo wa 8 wa Viongozi wa Afrika (ALF), chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi – Uongozi Institute siku ya Jumatatu ya Machi 7 mwaka huu na mkutano huo umeendelea tena Machi 8 mwaka huu nchini Uganda.