Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
SERIKALI imeteuwa timu maalum ya wataalamu kwa ajili ya kuishauri wizara ya Madini namna bora ya kuwainua wachimbaji wadogo wa madini ili kuzidi kuimarisha sekta ya madini ikiwemo kuwawezesha wachimbaji hao,kunufaika na rasilimali kwenye madini.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Madini Antony Mavunde katika mkutano na wadau wa sekta hiyo wenye lengo la kuisogeza mbele sekta ya madini ili kuwainua kiuchumi wachimbaji wadogo.
Mavunde alisema,timu hiyo imepewa muda wa mwezi mmoja kuwasilisha mapendekezo yake rasmi kwa Wizara, ambapo Waziri Mavunde amesisitiza kuwa serikali iko tayari kuyafanyia kazi mapendekezo hayo mara moja kwa lengo la kuongeza mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa.
Mavunde alisema timu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa wito kwa Wizara kuhakikisha sekta ya madini inapiga hatua huku wachimbaji wadogo wakichimba kwa tija na manufaa makubwa zaidi.
Alifafanua zaidi ya kuwa,serikali inafanya hivyo ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanainuka kiuchumi wao na familia zao,lakini pia wanaongeza wigo wa kuchangia pato la taifa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Serikali inahitaji kuona wachimbaji wadogo wanainuka kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija ambao unaleta matokeo chanya kwa jamii,”alisema Mavunde.
Mavunde alisema,kutokana na umuhimu wa Sekta hii ndogo ya uchimbaji madini alitumia nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Sera yetu ya Madini ya Mwaka 2009 imeweka bayana kuwa, mkakati wao ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini kwa kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kisasa sambamba na kuhakikisha wanakuwa na taarifa za kutosha za kijiolojia katika maeneo yao ya uchimbaji.
Alisema serikali,imeweka dhamira ya kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kupitia Sekta mbalimbali ambapo madini ni mojawapo na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini inakila sababu ya kuhakikisha kuwa, Sekta ya uchimbaji mdogo wa madini inaendelea kukuwa na inatoa fursa ya ajira kwa Watanzania.
“Ili sekta ya madini ikue kwa kasi na tija zaidi, ni lazima tuwape nafasi kubwa Watanzania katika kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi huu mnyororo,hii timu tumeiunda mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata msaada wa kitaalam, mitaji, maeneo ya uchimbaji na teknolojia ya kisasa ikiwemo kuweka mfumo mzuri wa kusaidia kutoka uchimbaji mdogo,kati mpaka mkubwa”alisema Mavunde
Ametaja Hadidu za rejea kwa timu timu hiyo kuwa ni pamoja na kupendekeza namna bora za kuwawezesha wachimbaji wadogo kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija,kutoa mapendekezo na kuendeleza wazo la kuundwa kwa Benki ya Wachimbaji Wadogo pamoja na Kupendekeza njia bora za kuanzishwa kwa Mfuko wa Madini kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wazawa.
Mavunde alisema,timu hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Victor Tesha (Makamu wa Rais, FEMATA), Katibu akiwa ni Dkt.Abdulrahman Mwanga (Kamishna wa Madini) huku Wajumbe wakiwa ni Theobald Sabi (Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC,Mwenyekiti wa Mabenki na Taasisi za Fedha), Ivan (Mtaalam wa Masuala ya Kifedha), Dkt. Mussa Budeba (Mkurugenzi Mtendaji wa GST), Hadija Ramadhani (Mwanasheria kutoka Tume ya Madini) na Dkt. Theresia Numbi (Mwanasheria na Mtaalam wa Local Content)
Naye Mwenyekiti wa Timu hiyo,Victor Tesha amesisitiza kuwa wanaenda kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na weledi mkubwa ili kulinda imani kwenye sekta ya madini kwa kuzingatia taaluma na uzoefu.