Na Mwandishi Wetu
Kikosi cha mpira wa pete cha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA Netball Club) kimetwaa ubingwa wa mashindano ya mpira wa pete ngazi ya Ligi Daraja la Tatu na hivyo kupanda Ligi Daraja la Pili.
Mashindano hayo ya ligi daraja la tatu Mkoa wa Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya TBS vilivyopo Ubungo Dar Es Salaam, yalishirikisha timu sita Timu zikiwemo: TBS, COMFORT, OSHA, BENJAMINI MKAPA S.S, DAR ZONE COMBINE NA MAKONGO SPORT ACADEMY.
Akizungumza baada ya mchezo wa mwisho, Kocha wa OSHA Netball Club, Bw. Ramadhani Maseka, ametoa pongezi kwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda kwa kuiwezesha timu kwa mahitaji mbalimbali ikiwemo kuipatia vifaa na motisha mambo yaliyopelekea timu yake kufanya vizuri na kufikia malengo ya Kupanda ligi Daraja la Pili na kuwa mshindi wa kwanza katika mashindano hayo.
Sambamba na hayo pia ametoa ombi kwa Mtendaji Mkuu wa OSHA kuendelea kuilea na kuiwezesha timu hiyo iweze kufika mbali kwa kuendelea kutwaa ubingwa wa michuano mbalimbali itakayo shiriki.
“Kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio tuliyopata kwani mashindano yalikuwa magumu lakini tumefanikiwa kuipandisha timu kutoka daraja la tatu mpaka daraja la pili,” amesema Bw. Maseka.
Kwa upande wake nahodha wa timu ya OSHA, Bi. Rachel Nkoma ametoa pongezi kwa wachezaji wote, viongozi wa taasisi wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA kwa jitihada walizofanya kuiwezesha timu kutwaa ubingwa.
Aidha, ametoa pongezi kwa vilabu mbalimbali ambavyo vimeshiriki katika mashindano hayo kwakua vilijipanga na vimeshiriki vizuri na kutoa ushindani mkubwa.
Timu ya OSHA ilishinda michezo yote mitano ambapo mechi ya kwanza iliifunga timu ya TBS kwa vikapu 44 kwa 20. Mechi ya pili ilikuwa dhidi ya Benjamini Mkapa ambapo OSHA ilishinda kwa jumla ya Vikapu 43 kwa 27. Matokeo ya michezo mingine yalikuwa kama ifuatavyo: OSHA dhidi ya Dar Zone (vikapu 52 kwa 37), OSHA dhidi ya Comfort (44 kwa 41) na OSHA dhidi ya Makongo (vikapu 61 kwa 7).