Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya Uhaini na kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha Umma.
Lissu amesomewa kesi ya uhaini chini ya kifungu cha sheria cha 39(2) cha kanuni ya adhabu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga na wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga.
Inadaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Katuga amedai kuwa siku ya tukio mshtakiwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo
“Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko….kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana.
Hata hivyo mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhaini ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na wameomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Hata hivyo upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wa Utetezi, Dkt. Nshala Rugemereza ulidai sheria inasema mtu afikishwe mahakamani upelelezi ukiwa umekamilika, lakini wanashangaa mteja wao amefikishwa mahakamani na wanaambiwa upelelezi bado.
Ibara ya 14 ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya mtu kuwa uhuru lakini inaonyesha upande wa mashtaka wana nia ovu kwani wanamkamataje mtu upelelezi ukiwa bado?
Tunaomba ama kesi ije kwa ajili ya kusikilizwa au mteja wetu aachiwe huru au apelekwe mahakamani pale upelelezi utakapokuwa umekamilika.
Wakijibu hoja hiyo, Wakili Katuga alidai kuwa ni kweli sheria inataka mtu kufikishwa mahakamani upelelezi ukiwa umekamilika lakini kuna kesi ambazo zinaweza kufikishwa mahakamani kutokana na usiriasi wake kama ilivyo kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga alikuballiana na hoja za upande wa mashtaka na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 24, 2025
Kesi ya pili, inayohusu mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni imesomwa na wakili wa serikali Harrison Lukosi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini.
Imedaiwa Aprili 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam mshtakiwa Lissu akiwa na lengo la kulangai umma alichapisha taarifa hizo kupitia mtandao wa YouTube ambapo maneno hayo yalisomeka ‘ Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana , wagombea wa Chadema walienguliwa kwa melekezo ya Rais.
Maneno mengine yalisomeka ‘ Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi, pia alichapisha maneno yaliyosomeka Majaji ni Ma-CCM hawawezi kutenda haki wanapenda wapate teuzi kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa’.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika hiyo Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24 mwaka huu Lisu atakaposomewa hoja za awali.
Katik kesi hii, Lisu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya sh milioni tano na kitambulisho cha Nida
