NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
MWEZESHAJI wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), Deogratius Temba amesema kunahaja kubwa wananchi kufuatilia na kusikiliza mijadala ya bajeti bungeni sambamba na kuhakikisha inaenda kuzungumza mahitaji halisi ya wananchi kama walivyojadili katika ngazi za mitaa pamoja na kata.
Ameyasema hayo jana April 09,2025 wakati wa Semina hiyo ambayo hufanyika kila jumatano katika viunga vya TGNP- Mtandao Jijini Dar es Salaam.
Amesema jamii inapaswa kufuatilia vipaumbele vyao kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kama vimetengewa fedha ili kutekelezwa na endapo havikupangiwa basi vitekelezwe kupitia rasimali zilizopo katika jamii kwa kushirikiana kati ya serikali ya mtaa na wananchi.
Kwa upande wake Mdau wa GDSS, Kidakule Wenseslaus ameishukuru serikali kutekeleza vipaumbele vyao mbalimbali katika eneo la Ilala-Jijini Dar es salaam ambapo ameeleza kuwa serikali imetekeleza katika sekta ya Afya, elimu pamoja na ulinzi.
Katika hatua nyingine,Kidakule amebainisha kuwa katika upande wa sekta ya maji katika eneo lao bado ni changamoto kwani hawajaona mradi mpya unaotekelezwa.
Naye Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Wilaya ya Ubungo,J amila Kisinga ameeleza kuwa katika bajeti iliyopita mengi yametelezwa ikiwemo ujenzi wa madarasa hata hivyo amesema wanatarajia bajeti ya mwaka 2025/2026 itakwenda kujibu hitaji la eneo lao kwa ujenzi wa Kituo Cha Afya ambacho eneo limetengwa kwaajili ya utekelezaji.