Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amezindua Kamati ya Kitaifa ya Ushauri Kuhusu Biashara ya Kaboni ikiwa na jukumu la kufanya tathmini na kutoa mapendekezo kuhusu njia bora na mwenendo wa biashara ya Kaboni nchini.
Amesema kwa kutambua umuhimu huo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeunda Kamati ya hiyo ya Kitaifa inayojumuisha wawakilishi kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Bianfasi ili kuongeza ufanisi katika kuratibu juhudi hizi na kuhakikisha tunapata matokeo chanya.
Waziri Masauni amezindua kamati hiyo Dodoma, Aprili 10, 2025 ambapo amesema Tanzania ina nafasi kubwa katika kuendeleza Biashara ya Kaboni na kuwa kinara katika sekta hii, lakini ili kufanikisha hilo, kunahitajika ushirikiano wa karibu.
“Pamoja na jukumu hilo lakini Kamati itafanya majukumu mengine kama vile kubaini na kuchambua changamoto za mfumo mzima wa biashara ya kaboni nchini kuanzia kwenye usajili, upimaji, uuzaji na makubaliano ili kuongeza uwazi na ufanisi na uwajibikaji.
“Kamati itaangalia masuala yanayohusu udhibiti wa biashara ya kaboni (Regulatory Environment), kushauri kuhusu biashara ya kaboni hususan katika kupata taarifa sahihi zitakazosaidia nchi kunufaika zaidi na mapato yatokanayo na biashara hiyo,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa kamati itashauri namna ambavyo maeneo yote muhimu ya kiuchumi yanafaidika na biashara ya kaboni ikiwemo miradi yote mikubwa ya kimkakati, kuchambua hali ilivyo ya usimamizi wa biashara ya Kaboni nchini pamoja na kutathmini Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini.
Aidha amesisitiza kuwa licha ya changamoto zilizopo, bado kuna fursa zitokanazo na mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari za mabadiliko ikiwemo biashara ya kaboni ambayo ni nyenzo muhimu ya motisha ya kupunguza uzalishaji wa gesijoto. Hivyo, ni wajibu wetu kuhakikisha tunatumia fursa ya miradi ya Biashara ya Kaboni inayochangia kupunguza uzalishaji wa gesi joto na uhifadhi wa mazingira ili kuchochea maendeleo.
Kwa kutambua umuhimu wa biashara ya kaboni, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeanzisha kisheria Kituo cha Taifa cha Kuratibu na Kusimamia Kaboni (NCMC) kupitia Marekebisho ya Sheria ya Mazingira yaliyoptishwa na Bunge tarehe 12 Februari, 2025 na kuidhinishwa na Serikali tarehe 4 Machi, 2025.
Baada ya Kituo cha NCMC kutambuliwa rasmi kisheria kama taasisi inayosimamia masuala ya biashara ya kaboni nchini, sasa inapaswa kuimarisha mifumo ya uratibu na usimamizi ili kuhakikisha miradi ya kaboni inatekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Wanaounda kamati hiyo ni Mwanahamisi Mbughi (Ofisi ya Rais – Ikulu), Hawa Mwechaga (Ofisi ya Rais – TAMISEMI), Kemilembe Mutasa (Ofisi ya Makamu wa Rais), Farhat Mbarouk (Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Kitengo cha Zanzibar), Dr Deo Shirima (NCMC), Grace Komba (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Pudensiana Protas (Wizara ya Mambo ya Ndani), Emilian Nyanda (Nishati), Gloria Ngaiza (Wizara Mbambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Prof. Dos Santos Silayo (TFS).
Wengine ni Bruno Mwaisaka (Tanganyikja DC), Augustino Mwakipesile (UDOM), Ephraimu Mdee (TRA), Hussein Mohammed (Mwanasheria wa Kujitegemea), Juma Kenene (BoT), Nicodemus D. Mkama (CSMA), Godfrey Marekano (TMX), Allan Lukindo (TNC), Amne Kagasheki (Shikana Group) na Ngenda kigaraba (COMEX Tanzania Ltd).