Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameupongeza mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuajiri Watanzania zaidi ya elfu sita wanaohudumu kwenye mradi huo mkubwa wa kimataifa.
Ametoa pongezi hizo Bungeni jijini Dodoma katika kikao cha pili cha mkutano wa 19 kwenye bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwasilisha muswada wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.
“Napenda kuupongeza mradi wa EACOP kwa kutoa ajira za muda kwa Watanzania 6610, pamoja na ajira za kudumu kwa watanzania 114, hiyo yote ni katika kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri kati ya mradi na wananchi wanaouzunguka mradi huu” amesema Waziri Mkuu.
Ameweka wazi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda zinatekeleza ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda mpaka mkoani Tanga nchini Tanzania kwa ajili ya usafirishaji kwenda katika masoko ya kimataifa.
“Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 55 na sehemu kubwa ya mradi huu unatekelezwa hapa nchini.Kati ya kilomita 1443, kilomita 1,115 zipo nchini Tanzania na tunajivunia sana uwepo wa mradi huu katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki” amesema.
Pia amesema Serikali ya Tanzania kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Mafuta Nchini (TPDC) ni mbia wa mradi huo wa EACOP na tayari wamekwishaweka kiasi cha dola za kimarekani milioni 376, ambazo ni sawa na kiasi cha hisa cha asilimia 15 ambacho kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania katika mradi huo.
Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.
Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Mradi huo umekuwa ukitoa ajira za aina mbalimbali ikiwemo za wataalam, wataalam wenye ujuzi wa kati na wale wasio na ujuzi kabisa ambapo kipaumbele cha ajira kwa kada hii hutolewa kwa watu wanaoishi karibu na mradi.