Dodoma. Tarehe 10 Aprili 2025: Baada ya ufanisi mkubwa kwenye mauzo ya Samia Infrastructure Bond yaliyohitimishwa mapema Januari, Serikali imewataka makandarasi kote nchini kuchangamkia mikopo iliyoanza kutolewa na Benki ya CRDB.
Utoaji wa mikopo hiyo uliozinduliwa na Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa jijini hapa itatolewa kupitia mfumo maalumu ujulikanao kama Samia Financing Portal, utawaunganisha wadau wote watatu yaani Benki ya CRDB, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mkandarasi hivyo kupunguza muda wa kushughulikia maombi ya mhusika.
“Ni fahari kubwa kuona mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia TARURA na Benki ya CRDB ambao kwa pamoja tulizindua Samia Infrastructure Bond mwishoni mwa mwaka jana. Fedha zilizopatikana kutokana namauzo ya hatifungani hiyo sasa zipo tayari kwa ajili ya kutekeleza malengo yaliyokusudiwa. Niwaombe makandarasi kuitumia vyema fursa hii wanapotekeleza miradi waliyoshinda,” amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri amesema ushirikiano baina ya TARURA na Benki ya CRDB unakusudi akuondoa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi kwa wakati ya barabara mijini na vijijini jambo litakalochangia kuharakisha maendeleo ya wananchi.
“Fedha zote kiasi cha shilingi bilioni 323 ziizotokana na mauzo ya Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond zitatumika kutekeleza miradi ya barabara inayosimamiwa na TAMISEMI.
Mfumo wa Samia Infrustructure Portal utarahisisha uchakataji wa maombi ya makandarasi ukitumia muda mfupi sana tofauti na ilivyo kwa mikopo mingine. Ni imani yangu na serikali kwa ujumla kuwa hali ya utekelezaji wa miradi itabadilika baada ya kuzinduliwa kwa mikopo hii itakayotolewa na Benki ya CRDB,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Mpaka tarehe 09 Aprili 2025, waziri amesema tayari imeshalipa madeni ya makandarasi zaidi ya 457 na malipo ya makandarasi wengine 322 yanakamilishwa na watalipwa na TARURA hadi kesho, Ijumaa ya tahere 11 ikiwa ni maelekezo ya Serikali kuhakikisha makandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini wamelipwa fedha zao na hawakwamishwi.
Kabla ya kumkaribisha waziri, Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Vaxery Makwi amesema benki imekamilisha utaratibu wa ndani na sasa ipo tayari kuanza kuwawezesha makandarasi kutekeleza majukumu yao bila kikwazo cha kifedha.
Makwi amesema makandarasi watawawezesha kupata dhamana za utekelezaji wa miradi wa kama dhamana ya utekelezaji wa mradi wakati wa utekelezaji wa zabuni (Bid Bond), Dhamana ya Utekelezaji wa Mradi (Performance Guarantee), na Dhamana ya Malipo ya Awali (Advance Payment Guarantee) na hati ya uthibitisho wa malipo (Letter of Credit).
Vilevile, watanufaika na mkopo wa kuanzisha mradi (bridge financing) mkopo wa bidhaa zinakazoagizwa kutoka nje (Post Import Loan), na uwezeshaji kupitia cheti cha malipo (Certificate Discounting).
“Ili kuhakikisha walengwa wanapata fedha kwa wakati, tumeandaa mfumo unaoitwa Samia Infrastructure Finance Portal unaopatikana kwenye tovuti ya Benki yetu ya CRDB pamoja na ile ya TARURA ambako makandarasi watatakiwa kujisajili ili kunufaika na uwezeshaji unaotolewa. Baada ya kujisajili, mkandarasi ataweka taarifa zake zote ambazo zitaenda TARURA kwa ajili ya uthibitisho, kisha taarifa hizo zitatumwa benki,” amesema Makwi.
Mfumo huo, Makwi amesema unamruhusu mwombaji kujisajili na kuomba mkopo autakao akiwa mahali popote pale bila kulazimika kwenda tawini hivyo kuokoa muda ambao anaweza kuutumia kufanya mambo mengine. Awali, amesema ilikuwa inamchukua mkandarasi mpaka mwezi mmoja kupata uthibitisho wa mradi anaouombea mkopo sasa hali imebadilishwa kupitia mfumo huo.
Ili kunufaika na mkopo wa makandarasi, mwombaji anatakiwa kuwa amesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB) katika daraja lolote, awe na mkataba halali wa mradi unaoendana na ukomo wa daraja lake kulingana na viwango vya CRB, awe na uzoefu wa kazi unaothibitishwa na angalau mradi mmoja aliowahi kuutekeleza kwa mafanikio, na awe na historia nzuri ya kukopa inayoweza kuthibitishwa.
“Napenda kuwajulisha makandarasi kuwa Benki yetu ya CRDB imejipanga viliyo kutoa mikopo hii kupitia matawi yetu yaliyopo kote nchini. Wafanyakazi wetu wameandaliwa ipasavyo na wana ujuzi wa kutosha kuhakikisha huduma hii inatolewa kwa ufanisi na kwa haraka. Katika kila tawi, kuna timu maalum kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu. Nawawakaribisha makandarasi kote nchini kutumia fursa hii ili kukamilisha miradi wanayoitekeleza,” amesema Makwi.