Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Songea SOUWASA, imeanza utekelezaji wa mradi wa maji wa Londoni Sinai, wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5, chini ya Mkandarasi Estate Constructors Limited, mradi unaotarajiwa kukamilika ndani ya siku 365.
Akikabidhi mabomba ya usambazaji maji katika eneo la Sinai Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea, Kaimu Meneja wa uendelezaji Miundombinu kutoka SOUWASA Eng. Vicent Bahemana amewataka wananchi kuwa na uchungu nakuona thamani ya miundombinu hiyo kwa kuilinda ili kuepuka baadhi ya wananchi kukosa uwezekano wakufikiwa na maji kama utatokea wizi wa mabomba ambayo yalikusudiwa yasambazwe ili maji yawafikie wananchi wote.
Bahemana amewataka wananchi wa Sinai na Mang’ua kuwa wavumilivu wakati mradi huo unatekelezwa kwani ni dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo, ambapo wanatarajia kulaza mabomba kilometa 44.9 ikiwa wamelenga maeneo yote ya makazi ya watu kwani wamezingatia zaidi vipaumbele katika maeneo yote yakutolea huduma za kijamii zikiwemo shule, makanisa, hospitali, misikiti n.k.
Diwani wa Kata ya Lilambo Yobo Mapunda, ameipongeza Mamlaka na Serikali kwa ujumla kuanza utekelezaji wa mradi huo kufuatia uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Sinai na Mang’ua, huku akieleza kuwa wananchi wanadeni kwa Rais Samia la kumpigia kura uchaguzi Mkuu mwaka huu kufuatia utekelezaji wa ilani ya CCM kwenye eneo hilo.
Kwa upande wa Wananchi nao hawakusita kutoa pongezi zao kwa serikali kufuatia ujenzi wa matenki ya maji na mabomba hayo kufikishwa eneo hilo huku matarajio yao nikuepuka kutembea umbali mrefu kufuata maji na kupata magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakijitokeza.