Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MDAU wa maendeleo wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Taiko Kulunju Ole Tipa Munimuni ametoa msaada wa matenki matatu ya kuhifadhi maji ya ujazo wa lita 15,000 yenye thamani ya shilingi milioni 3.
Matenki hayo matatu ambayo kila moja ina ujazo wa lita 5,000 ambapo moja limepelekwa shule ya sekondari Loiborsiret kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na walimu na mawili yamepelekwa katika kitongoji cha Oltepeleki kwenye changamoto ya upungufu wa maji.
Matenki hayo matatu ya kuhifadhi maji yamekabidhiwa na Joseph Siria kwa niaba ya Taiko, kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Oltepeleki, Rise Laarmadat na afisa mtendaji (VEO) wa kijiji cha Loiborsiret Upendo Menasi.
Kwa upande wake, Joseph Siria akizungumza kwa niaba ya mdau wa maendeleo, Taiko amesema mchango huo ni sehemu ya dhamira yake ya kusaidia jamii anayoipenda na kuishi nayo ili ipige hatua kimaendeleo.
“Natoa wito kwa jamii na wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa Taiko ambaye amekuwa na moyo mkunjufu wa kujitolea katika suala zima la maendeleo,” amesema.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho Menasi ametoa shukrani za dhati kwa mdau huyo wa maendeleo kwa moyo wa uzalendo na upendo mkubwa alionao kwa jamii.
Ametoa ahadi ya kuhakikisha matenki hayo matatu yanatunzwa na kulindwa ipasavyo huku yakitumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, wamemshukuru Taiko kwa kujitolea msaada huo kwa jamii kwa kuwapa matenki hayo matatu ya kuhifadhi maji.