Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewaomba radhi wateja wake wa mikoa ya Ruvuma, Songwe, Mbeya, Njombe na Wilaya ya Masasi, kufuatia kukosekana kwa huduma ya umeme kesho Jumamosi ya Aprili 12, 2025, Katizo hilo litaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO Makao Makuu – Dodoma, sababu ya katizo hilo ni matengenezo kinga ya mitambo katika kituo cha kupoza umeme cha Makambako.
Matengenezo hayo yanalenga kuboresha ufanisi wa mitambo na kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa wateja wanaohudumiwa na kituo hicho, Kutokana na kazi hiyo ya kiufundi, katika maeneo ya mikoa husika yatakumbwa na ukosefu wa umeme kwa muda uliotajwa.
TANESCO imewahakikishia wateja wake kuwa matengenezo hayo ni ya muda mfupi na yatachangia katika utoaji wa huduma bora zaidi kwa siku za usoni, Shirika hilo pia limewaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati wa kipindi chote cha matengenezo.