Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. David Cosato Chumi (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ametoa wito
kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuchangamkia fursa ya kuwekeza
nyumbani, akisema kuwa mchango wao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Akaunti ya Mzawa, huduma maalum ya kifedha kwa diaspora
iliyozinduliwa na Benki ya Absa Tanzania.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhe. Chumi ameipongeza Benki
ya Absa kwa ubunifu wa huduma hiyo ambayo inalenga kupunguza changamoto
wanazokutana nazo Watanzania wanaoishi ughaibuni, hususan katika kupata huduma
za kifedha, kutuma fedha, na kushiriki katika uwekezaji wa ndani.
“Akaunti hii ni suluhisho la changamoto za kifedha kwa
diaspora. Inawaruhusu kufungua akaunti, kutuma fedha, kuwekeza, na kutumia
sarafu 5 tofauti wakiwa popote duniani.
Amefafanua kuwa mchango wa diaspora umekuwa ukiongezeka kila
mwaka, akitaja kuwa mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio nje walituma nchini
fedha za kigeni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.4. Amesema fedha
hizo zimechangia maendeleo ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, biashara, na
ujenzi wa makazi.
“Serikali inatambua nafasi muhimu ya diaspora. Ndiyo maana
tumekamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje inayojumuisha masuala ya
diaspora, tumeanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili wa diaspora, tumepitisha
hadhi maalum kwa Watanzania wasio raia, na kuanzisha vitengo mahsusi serikalini
vya kushughulikia masuala yao,” ameongeza Mhe. Chumi
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa
Tanzania, Bw. Obedi Laizer, amesema huduma hiyo imebuniwa kwa kuzingatia maoni
ya Watanzania waishio nje, na kwamba benki hiyo itaendelea kushirikiana na
Serikali katika kukuza uwekezaji wa ndani na biashara jumuishi.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya
Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Salvatory Mbilinyi, mabalozi
wastaafu, na wadau mbalimbali wa sekta ya kifedha na uwekezaji.