Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyika jijini Dodoma
Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamepongezwa kwa kuandaa na kuendesha kwa mafanikio makubwa mkutano mkuu wa mwaka, hatua ambayo imewawezesha kujadili kwa kina taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na kuweka mapendekezo yenye lengo la kuongeza tija ndani ya TCAA.
Akifungua rasmi mkutano huo wa siku mbili uliofanyika jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya aliwapongeza viongozi wa TUGHE TCAA kwa uendeshaji mzuri wa shughuli za chama kwa namna shirikishi, akieleza kuwa tawi hilo limekuwa mfano bora wa kuigwa na matawi mengine.
“Nawasihi viongozi waendelee kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE kwa sababu huo ndio uhai wa chama. Bila wanachama hai, hakuna chama hai. TCAA mmeonyesha njia nzuri, endeleeni kushikamana na kushirikiana,” alisema Ndg. Msuya.
Kwa upande wake, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sara Rwezaura aliwataka wanachama wa TUGHE TCAA kuwa wavumilivu wakati wa kuwasilisha hoja zao, na kusisitiza kwamba hoja zao ni muhimu na zisikaliwe kimya bali ziwasilishwe kwa mujibu wa taratibu.
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA, Bi. Jackline Ngoda aliwashukuru viongozi wenzake kwa kuendelea kudumisha mshikamano ndani ya uongozi na kuahidi kuongeza nguvu katika kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE.
Naye Katibu wa TUGHE TCAA, Bw. Shukuru Mhina alisisitiza umuhimu wa mafunzo kwa viongozi wapya wa TUGHE akieleza kuwa ni kupitia mafunzo ndipo viongozi bora hujengwa.
Mkutano huu wa mwaka wa TUGHE TCAA umeendelea kuonesha mfano wa uwajibikaji, mshikamano na ushirikishwaji, hali inayoendelea kuimarisha misingi ya utendaji bora ndani ya taasisi.
Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula akitoa salamu za TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyika jijini Dodoma
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bi. Jackline Ngoda akizungumza kuhusu namna wanavyoshirikiana na viongozi wa TCAA pamoja na kumkaribisha Mgeni rasmi.
Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Bw. Shukuru Mhina akifanywa utambulisho wa wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA
Wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA wakiwasilisha michango wakati wa mkutano
Nsubisi Mwasandende Afisa Elimu Kazi na Mratibu wa Jinsia TUGHE akiwasilisha mada kuhusu mbinu za usajili na kuwatunza wanachama kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA
Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).