Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akisaini maadili ya Uchaguzi kwa niaba ya Tume.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi akisaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya Serikali.Vyama 18 vya siasa vyenye
usajili kamili, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wamesaini Kanuni za
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 leo tarehe 12
Aprili, 2025 jijini Dodoma.
Vyama hivyo ni pamoja na Chama
cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), National Convention for
Construction and Reform (NCCR), Union for Multiparty Democracy (UMD), National
League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National
Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA).
Vyama vingine ni Tanzania
Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI),
Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party
(AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama
cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Alliance for Change and Transparency
(ACT-Wazalendo).
Kwa upande wa Serikali Kanuni
hizo za maadili zilisainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge
na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi na kwa upande wa Tume alisaini Mwenyekiti wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele.
Awali akizungumza kabla ya utiaji
saini, Jaji. Mwambegele alivishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano wao wakati
wote wa uandaaji wa kanuni hizo za maadili.
“Tunawashukuru viongozi wote
wa Vyama vya Siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano Tume katika
utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali hususan yale yanayohusu mchakato wa
maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo uandaaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi
ambazo tupo hapa leo kwa ajili ya kutia saini kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani wa mwaka 2025,” alisema Jaji Mwambegele.
Amesema Tume imeandaa kanuni
hizo za maadili ambazo zitatambulika kama Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha
162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024.
“Baada ya kukamilisha
maandalizi ya rasimu ya Kanuni hizo, Tume iliziwasilisha kwenu (vyama vya siasa
na Serikali) kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yenu kuanzia tarehe 1 Machi,
2025 hadi tarehe 14 Machi, 2025. Maoni
yenu yamejumuishwa katika Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani za Mwaka 2025 tutakazotia saini hii leo. Napenda kutoa shukrani za dhati kwenu kwa
ushiriki wenu katika kuandaa rasimu hiyo kwa kutoa maoni yenu na kuyawasilisha
Tume kwa wakati,” alisema Jaji Mwambegele.
Aliongeza kuwa baada ya
kukamilisha rasimu ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani za mwaka 2025, Tume iliwarejeshea tena wahusika Rasimu ya Kanuni hizo
tarehe 4 Aprili, 2025 na kuwaalika kwa ajili ya utiaji saini leo tarehe 12
Aprili, 2025 na kwamba hakuna maoni tofauti yaliyotolewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu Kailima, R. K wakati akifafanua
mambo muhimu yaliyomo kwenye kanuni hizo amesema vyama vya siasa vina wajibu wa
kufanya kampeni za kistaarabu na kujiepusha na mambo yanayoweza kupelekea
uvunjifu wa amani.
Ameongeza kuwa Serikali kwa
upande wake ina wajibu wa kutoa fursa sawa ya vyama vya siasa kufanya kampeni,
kutumia vyombo vya habari vya umma na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na hali ya
utulivu na amani.
Kwa upande wa Tume, Kailima
amesema inawajibika kwenye mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchaguzi
unakuwa wa huru na wa haki na kuhakikisha kunakuwa na usawa katika mchakato wa
uchaguzi.
Amesisitiza kuwa chama ambacho
hakijasaini maadili hayo hakitopata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu na
chaguzi ndogo nyingine zote zitakazofanyika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.