Na Karama Kenyunko – Michuzi Blog
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza kuwa kuanzia Mei Mosi, 2025 itasitisha matumizi ya namba za vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wote waliotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) wa kwenda kuchukua vitambulisho vyao lakini hawajajitokeza kuvichukua.
Akizungumza leo Aprili 14, 2025 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji alisema kuwa tangu zoezi hilo lianze Januari mwaka huu hadi Machi 23, 2025, wananchi 1,880,608 walikuwa bado hawajachukua vitambulisho vyao, lakini waliotii wito huo na kuchukua vitambulisho ni 565,876 sawa na asilimia 30.
“NIDA imesikitishwa na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kuchukua vitambulisho vyao licha ya kutumiwa ujumbe wa kuwataarifu mahali pa kuvichukua. Hivyo tumeamua kusitisha matumizi ya namba za vitambulisho kwa wale waliotumiwa SMS lakini hawajajitokeza,” alisema Kaji.
Aliongeza kuwa kuanzia sasa mtu anaposajiliwa, ndani ya siku tano atapokea ujumbe wa namba yake ya NIDA, na ndani ya siku 21 ujumbe mwingine utatumwa kumwelekeza mahali pa kuchukua kitambulisho. Akishindwa kufanya hivyo ndani ya mwezi mmoja, namba yake itafutwa.
“Tunatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatunza ujumbe huo na kuenda nao katika ofisi za NIDA ili kuepusha usumbufu,” alisisitiza.
Amesema pia NIDA inafikiria uwepo wa faini kwa wale watakaoshindwa kufuata utaratibu huu, hasa ikizingatiwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kutoa huduma hiyo bila malipo.
Kaji pia amewashauri vijana wanaofikisha miaka 18 kujisajili mapema badala ya kusubiri hadi wakati wa ajira, ambapo mara nyingi hujitokeza kwa wingi na kusababisha misuguano na wafanyakazi wa NIDA.
Ameeleza kuwa NIDA inaendelea kuboresha mifumo yake kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na taarifa sahihi na salama. Pia, amekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kuhusu NIDA kusajili bima ya Toto Afya Card akisema kuwa hiyo si kweli na NIDA haina usimamizi wowote juu ya suala hilo.
Aidha, ameeleza kuwa kwa maelekezo ya Waziri mwenye dhamana, sasa kila eneo lenye ofisi ya NIDA linapaswa kuwa na afisa uhamiaji kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa wananchi.
Kuhusu vitambulisho vilivyofutika, amesema tayari suala hilo limepatiwa ufumbuzi kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadhi ya wananchi wameanza kupewa vitambulisho vipya. Amewataka wananchi kujaza fomu kwa usahihi ili kuepuka makosa ya majina na taarifa nyingine.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) James Kaji akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 14, 2025 ofisini kwake jijini Dar es Salaam