Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Kampuni ya Ntandothando Group ya Johannesburg, Afrika Kusini imeonesha nia ya kuwekezai katika mradi wa Green Smart City, eneo la Njedengwa jijini Dodoma mradi ulio chini ya Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina Saccos)
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Dkt. Festo Mwaipaja wakati wa Mkutano na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Uwekezaji ya Ntandothando Group, Bw. Lucas Mteto.
Alisema kuwa wamefanya mazungumzo na Mwekezaji na kutembelea eneo husika ambapo amevutiwa na eneo hilo kwa kuwa linaendana na maono ya Kampuni hiyo ya kuwekeza kwenye miradi inayozingatia uhifadhi wa mazingira.
“Mradi huu kama ukikamilika una manufaa makubwa kwa Taifa kwa kutekeleza agenda ya kutunza mazingira, kuongeza mapato kwa njia ya kodi, ajira na kuwa Saccos ya kwanza kuunga jitihada za Mhe. Rais katika suala la utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kuweka mifumo itakayokabiliana na uchafuzi”, alieleza Dkt. Mwaipaja.
Alisema kuwa mradi huo utakuwa na faida kwa Wanachama wa Saccos hiyo kwa kuwa watapata mgao kupitia faida itakayopatikana, kupunguza riba ya mikopo ya wanachama na Chama kuwa na chanzo kingine cha mapato, uendelevu wa chama na pia itasaidia upatikanaji wa huduma kwa jamii inayozunguka eneo la mradi.
Alisema kuwa Hazina Saccos ilifanya upembuzi yakinifu wa eneo la uwekezaji na kubaini uwekezaji utakuwa na tija kwa Saccos, wawekezaji na nchi kwa ujumla.
Dkt. Mwaipaja alisema Chama hicho kilibuni mambo mbalimbali ili kupata kipato nje ya riba kutoka kwa wanachama, hivyo mwaka 2014 Bodi ya Hazina Saccos ilitafuta eneo la uwekezaji eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.
Alisema ili kuweza kumpata mwekezaji mwenye tija, Bodi ya Hazina Saccos ilitengeneza chombo huru kitakachosaidia upatikanaji wa mwekezaji kwa kuunda Kamati iliyojumuisha wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali za umma.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Ntandothando Group ya Johannesburg, Afrika Kusini, Bw. Lucas Mteto, alisema amekuwa na mazungumzo mazuri na Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos na Mwenyekiti wa Uwekezaji wa eneo la Njedengwa baada ya kutembelea eneo hilo.
Alisema kuwa eneo la Uwekezaji ni zuri na linafaa kwa uwekezaji ambao unazingatia uhifadhi wa mazingira na pia kuwa na uwekezaji wa mfano katika jiji la Dodoma, alisema Kampuni ya Ntandathando Group imekuwa ikitekeleza miradi katika maeneo mbalimbali barani Afrika kwa manufaa ya Kampuni na wananchi wa eneo husika.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mradi wa Njedengwa, Prof. Ester Ishengoma, kutoka Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema Kamati imefurahi kwa kuwa mwekezaji anaonesha nia ya dhati ya uwekezaji wenye tija.
Alisema wameanza hatua za awali za mchakato wa uwekezaji ambazo ni pamoja na kuona eneo la uwekezaji na kufanya majadiliano ya namna ya utekelezaji wa mradi huo.
Alisema mwekezaji aliyepatikana kwa sasa ambaye ni Kampuni ya Ntandothando Group ya Afrika Kusini, pamoja na mambo mengine, inajihusisha na masuala ya ujenzi, kilimo na Mifumo ya Tehama.






Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Dkt. Festo Mwaipaja, (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mradi wa Njedengwa, Prof. Ester Ishengoma (wa tatu kushoto) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Uwekezaji ya Ntandothando Group ya Afrika Kusini, Bw. Lucas Mteto, (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa eneo la Njedengwa, linalomilikiwa na Hazina Saccos, baada ya mkutano kati yao, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha)