Na Mwandishi wetu
Nyumba zaidi ya 350 za makazi bora na gharama nafuu,zimejengwa hapa nchini kwa ajili ya kusaidia makazi ya watu wenye kipato duni ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maisha ya jamii katika maeneo mbalimbali.
Nyumba hizo zimejengwa na Shirika lisilo la kiserikali la Habitat for Humanity Tanzania katika mikoa 13 ya Bara na Visiwani ikiwa ni jitihada za kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo tofauti hapa nchini.
Mbali na hilo,shirika hilo limezifanyia maboresho nyumba zaidi ya 300,ikiwemo kuzikarabati ili kuhakikisha zinakuwa na mtazamo halisi wa nyumba ta kuishi watu
Mpango huo wa kujenga nyumba hizo ulibainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mradi wa Ujenzi wa Makazi bora,ya gharama nafuu na endelevu,John Masenza katika kijiji cha Dabalo kilichopo halmashauri ya Chamwino mkoani hapa,liliienda sambamba na uonyweshwaji eneo la ujenzi kwa Mkandarasi.
Amesema,Shirika hilo limeitikia wito wa serikali wa kushirikiana na Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,ikiwemo uboreshwaji wa makazi ya watu ili kuhakikisha Jamii inaishi katika mazingira bora.
Alitaja mikoa ambayo nyumba hizo zimejengwa ikiwemo kuziboresha ni Kigoma,Tabora,Mwanza,Iringa Tanga,Ruvuma,Morogoro,Arusha ,Manyara,Dodoma,Dar es Salaam,Pwani na Zanzibar.
Masenza amesema zaidi ya wanufaika 189,000 wamenufaika na ujenzi huo katika maeneo mbalimbali hapa nchini,huku akisisitiza mradi huo ni endelevu.
“Shirika litaendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,ikiwemo ya elimu,Afya na Maji ili kuhakikisha inafikia malengo iliojiwekea,”alisema Masenza.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa Nyumba 10 za walengwa wa kijiji cha Dabalo kilichopo halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma,alisema zitagharimu shilingi milioni 500 ambapo familia husika zitakadhiwa mara ujenzi huo utakapokamilika.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Chamwino Justina Amo aliwaagiza viongozi wa serikali ngazi ya vijiji,kuhakikisha wanawasilisha watu ambao wanavigezo na si kuleta udanganyifu katika zoezi hilo la kupata walengwa.
Amesema wanalishkuru shirika hilo kutokana na kutoa msaada huo kwa wakazi wa eneo hilo la Dabalo,huku akisisitiza viongozi wa kijiji cha Dabalo kutoa ushirikiano pindi zoezi la ujenzi huo linapoendelea.
“Nawashkuru sana Habitat for Humanity Tanzania kwa utekelezaji wa mradi huo,serikali kupitia viongozi wa kijiji watasimamia vizuri kuhakikisha nyumba zinakamilika,” Amo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Dabalo Abeid Athanas aliwataka shirika hilo kutokuwa na wasiwasi wowote ule huku akiwahakikishia serikali itaendelea kushirikiana nao,kuhakikisha mradi huo unakamilika.