Mwandishi Wetu
TAASISI ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), imetaja mafanikio ya miaka manne chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuwapatia chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi watoto wa kike milioni 1.2 wenye umri wa miaka tisa hadi 14
Mafanikio mengine ni kupokea fedha Sh. bilioni 40 kutoka Serikalini kwa lengo la kubadilisha miundombunu ya matibabu kwa kununua mashine za kisasa za ugunduzi wa saratani.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI Dk. Diwani Msemo, amesema taasisi hiyo ilianzishwa miaka 30 iliyopita, mambo mengi yalifanyika lakini chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yamefanyika maboresho mbalimbali ikiwemo taasisi hiyo kupata vifaa tiba vya kisasa na kuongezewa wafanyakazi.
Dk. Diwani amesema kwa kipindi cha miaka minne taasisi hiyo imehimarisha huduma za uchunguzi kwa kununua vifaa vya kisasa vya picha ikiwemo xray za digitali.
“Ugonjwa wa saratani ni tatizo kubwa kwa jamii ndio maana serikali mara kwa mara inatoa fedha kwa lengo la kufanya ununuzi wa vifaa vya kisasa vinavyohusiana na ugonjwa huo.
Kuhusu huduma za mikoba zinazotolewa katika taasisi hiyo Dk. Msemo amesema ni moja ya mafanikio yao katika kipindi cha miaka minne.Huduma hiyo ya mkoba imekuwa msaada kwao kwa sababu husaidia kugundua watu wenye saratani kwa hatua ya awali .
Aidha Dk. Msemo amesema lengo lao ni kuwapima na kuona kama wanaviashiria vya saratani wanatoa huduma za matibabu ya awali
“Tumeanza kuzunguka mikoa mbalimbali nchini na tumeshapima watu 80,000 kati ya hao watu 10,000 wali gundulika na saratani na tayari wameshaanza matibabu ya awali.Dk.Msemo alisema kesho wanapeleka huduma zao katika mikoa ya nyanda za kusini ikiwemo Ruvuma, Mtwara na Kigoma.
Kuhusu Ocean Road amesema taasisi hiyo ni bingwa katika nchi za jangwa la sahara kwa kuwa na vifaa vya kisasa na kusisitiza vipimo vinavyotoka katika taasisi hiyo vinakubalika katika hospitali za nje ya nchi kwa sababu mashine zinazotumika ni za kisasa.
Aidha amesema kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Serikali imeweza kuongeza wafanyakazi wapya asilimia 55 huku madaktari bingwa wakiwa 40.