Na Diana Byera,Missenyi
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuwa wananchi wasiwe waoga kuwasema hadharani Waharifu wanaofanya dhuruma kwenye jamii zao pamoja na unyanyasaji unaoambatana na ukatili kupitia kampeini ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia
Akizungumza na wananchi wa kata ya Nsunga wilayani Missenyi mkoani Kagera, alisema kuwa muda wa kusema waharifu ni sasa kwani kampeni ya msaada wa Kisheria wa Mama Samia haitaacha changamoto yeyote ya Mwananchi inayohusu maswala ya Kisheria.
” Muda wa kuwasema waharifu hadharani ni sasa ,baadhi ya watu ni wanyanyasaji ,wengine wamenyanga’nya watu Ardhi ,kunyanyasa wajane ,ubakaji na ulawiti ,nataka kuwahakikishia wananchi kuwa Kampeni ya kisheria ya mama Samia haitaacha Changamoto yoyote inayohusu Sheria sisi tunasema ni Haki,usawa ,na Maendeleo “amesema Ndumbaro
Amesema kuwa kipindi cha nyuma wananchi walikuwa Wakiwatafuta wanasheria na mawakili kufuata huduma za kisheria lakini kwa sasa Wanasheria na mawakili ndio watawafuata wananchi kwenye vijiji vyao, lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Watanzania kupata haki zao kwa wakati sahihi na kuondokana na adha ya gharama kubwa za kuendesha kesi.
Aidha amesema tayari serikali imejenga jengo la mahakama katika wilaya ya Missenyi,jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwa miaka yote wilayani Missenyi hivyo anaamini uwepo wa jengo la mahakama umerahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi ambao walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata haki za mahakamani wilaya ya Bukoba.
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Katiba na Sheria Frankilini Rwezimula amesema kuwa Huduma za kisheria kupitia kampeni ya mama Samia itadumu katika wilaya ya Missenyi kwa siku 9, ambapo Kila siku timu itasikiliza kero na changamoto za kisheria vijiji vitatu kwa siku ,ndani ya Kata kwa siku moja.
“Naomba wananchi tujitokeze kwa wingi kuleta kero zetu za kisheria ili zipate ufumbuzi ,lakini sio kero tu hata Elimu ya kisheria kujua swala lako litaenda wapi lakini pia serikali inakusaidia kupata wanasheria watakakusaidia kupata majawabu ya haki zao ,tusiwe wakimya kwa mambo yanayotuumiza”amesema Rwezimula.
Mbunge wa Jimbo la Nkenge Frolent Kyombo amesema kuwa Uwepo wa kampeni hii ni tunu na Fursa kwa wananchi wa wilaya ya Missenyi kwani wananchi wengi hawana uwezo wa Kujiwekea wanasheria na kuwaghamia.
Amesema anaamini wananchi wa wilaya ya Missenyi kupitia kampeni hii watatatua changamotoo zao zinazowakabiri ,kwani baadhi ya wananchi kesi zao zimeshindwa kuendelea kutokana na kutokuwa na gharama za kuwalipa mawakili ambapo amewahakikishia wananchi wa Missenyi kuwa Kampeni hii ya kisheria ina majawabu yao yote hivyo wasikose kujitokeza.
Halikadhalika ameishukuru serikali kwa kujenga jengo la mahakama katika wilaya ya Missenyi kwani wananchi wengi wanyonge walikuwa hawana uwezo wa kusafiri kwenda mahakama ya wilaya ya Bukoba ,hivyo uwepo wa mahakama ndani ya wilaya hiyo ni sehemu ya wananchi kupata haki kutokana na chombo hicho kutoka haki kwa Kila mtu.