SHIRIKA lisilo la kiserikali la Smile for Community (S4C) kwa kushirikiana na LSF leo limetangaza msimu wa nne wa mbio za Run for Binti zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Mei 2025 katika viwanja vya Farasi,Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Mbio hizi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuweka nguvu na rasilimali za pamoja katika kuwawezesha watoto wa kike kupata haki ya elimu na afya ya uzazi, kwa kuhakikisha wanapata hedhi salama na mazingira bora ya kusoma.
Kupitia Run for Binti ya mwaka jana, wanafunzi wa shule za sekondari Nanyamba na Chawi katika Halmashauri ya Mji Nanyamba walinufaika kwa kujengewa vyoo bora na vya kisasa, huku wanafunzi wa kike wakipata taulo za kike kwa ajili ya kuwalinda kiafya na kuwawezesha kuhudhuria vipindi bila kukosa.
Akizungumza wakati wa kutangaza mbio hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema “Katika utekelezaji wa mradi wetu wa Sauti ya Mwanamke nchini, tumeona dhahiri kwamba wasichana na mabinti wanakumbana na vizuizi vinavyozuilika na visivyoweza kuzuilika katika kupata elimu, huduma za afya, na haki zao za msingi. Ndiyo maana ushirikiano wetu na Smile for Community pamoja na wadau mbalimbali ni muhimu sana. Kupitia mbio hizi, tunapunguza vikwazo na kutengeneza njia mpya zitakazochochea jamii yenye usawa hususan kwa mtoto wa kike.”
Aidha amesema mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa la kuwaleta wadau pamoja na kuweka nguvu ya pamoja kutatua changamoto za watoto wa kike.
“Mwaka jana, zaidi ya wanafunzi 2,500 walinufaika kupitia ujenzi na ukarabati wa vyoo, usambazaji wa taulo za kike, upandaji wa miti mashuleni na utoaji wa elimu ya hedhi salama na haki za mtoto wa kike”. Amesema
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Smile for Community, Bi Flora Njelekela amesema “Smile for Community kwa kushirikiana na LSF tuna furaha kubwa kutangaza kuwa mbio za msimu huu wa nne zitafanyika tarehe 24 Mei 2025. Wakimbiaji watahusika katika mbio za KM 21, KM 10, KM 5.”
Bi Njelekela ameongeza kuwa, “Lengo letu mwaka huu ni kufikia watoto wa kike 1,000 kutoka shule tatu, hasa mikoa ya Geita na Dar es Salaam. Katika tukio la makabidhiano, msaada utakao tolewa utahusisha: Usambazaji wa taulo za kike 7,000, Ujenzi wa vyoo bora mashuleni, Upandaji wa miti 500 katika shule tatu kwa ajili ya hifadhi ya mazingira, Elimu ya ukatili wa kijinsia na mbinu za kuzuia na kushughulikia matukio hayo, Elimu ya fedha (financial literacy) na Uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking), lakini pia Shughuli za mazingira zitafanyika Ukonga, Dar es Salaam na shughuli za afya ya hedhi, elimu ya fedha na miundombinu Geita.”