Farida Mangube, Morogoro
Changamoto ya kuoza na kuharibika kwa mazao ya bustani kumewasukuma wanafunzi wabunifu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuja na ubunifu wa kifaa ambacho kina uwezo wa kutunza mazao hayo kwa muda mrefu zaidi.
Mwanafunzi Christina Josephat anayesoma Shahada ya Sayansi ya Usalama wa Chakula na Uthibiti Ubora, SUA amesema wamekuwa wakiguswa na namna ambavyo wafanyabiashara wanapata hasara ya kuoza kwa mazao ya matunda na mbogamboga kiasi cha kulazimika kuuza hata kwa bei pungufu hasa majira ya joto.
“Tuliguswa sana na hali hiyo, ndipo tulipoanza kuulizana sisi wenyewe kwamba tunaweza kufanyaje, ndipo tukaamua kuja na wazo na kifaa hiki rahisi lakini chenye msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo maana hakitumii umeme,” alisema Christina.
Christina ambaye anaiwakilisha Kampuni ya Fruit Secure Solution ambayo imezalisha kifaa hicho anasema ujio wake utakuwa msaada kwani kinauwezo wa kutunza matunda bila kuoza kutoka wastani wa siku 3 hadi 9 jambo ambalo litapunguza hasara na kuongeza tija kwa wafanyabiashara.
Kampuni ya Fruit Secure Solution ilitangazwa mshindi wa kwanza katika shindano la ubunifu lililoandaliwa na SUA Innovation Hub, jambo lililothibitisha ubora na mchango wa mradi huo katika sekta ya kilimo na lishe nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Lucia Madalla kutoka Kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia na Kituo cha Ubunifu SUA alisema kuwa kitengo kitaendelea kukuza na kulea wanafunzi wenye bunifu ili waweze kukua na kuleta suluhisho kwa changamoto.
“Tunaendelea kuwalea wanafunzi ili waendeleze bunifu zao kwa manufaa yao binafsi hata kwa taifa kwa ujumla,” alisema Bi. Madalla.
Fruit Secure Solution inaendelea kupanua wigo wake katika masoko mbalimbali ya ndani nchini Tanzania, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kupunguza upotevu wa chakula na kulinda mazingira.