Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Mohamed kushoto akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitangaza mkutano wa uwekezaji wa vitega uchumi kwa mwaka 2025. Mkutano huo utafanyika katika Kisiwa cha pemba kwa siku tatu kuanzia Mei 7 hadi 10.
MAMLAKA ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imetangaza kuwa Mkutano wa Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar kwa mwaka 2025 utafanyika katika Kisiwa cha Pemba kuanzia Mei 7 hadi 10, kwa lengo la kuhamasisha fursa mpya za uwekezaji visiwani humo. Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Ni Wakati wa Pemba.”
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Aprili 17, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, amesema mkutano huo ni hatua kubwa katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inayolenga kulifanya Kisiwa cha Pemba kuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
“Mkutano huu ni zaidi ya tukio; ni hatua ya mabadiliko kwa ushirikiano wa ndani na wa kimataifa ambao utaunda mustakabali wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla,” amesema Saad.
Amebainisha kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa la kipekee kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali, hasa katika sekta zenye kipaumbele kama uchumi wa bluu, kilimo, utalii, nishati mbadala, na viwanda vya bidhaa mbalimbali.
Mkutano huo unatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 750 wakiwemo wakurugenzi, wakuu wa makampuni makubwa, wawekezaji wa kimataifa, viongozi wa serikali na wanadiplomasia.
Aidha, kutakuwa na mijadala ya hali ya juu, maonyesho ya biashara kwa muda wa siku mbili, ziara za kuhamasisha jamii, pamoja na hafla maalum ya wawekezaji itakayoandaliwa na Rais Dk. Mwinyi.
ZIPA pia imetoa wito kwa sekta binafsi, taasisi za umma, mashirika ya kimataifa ya maendeleo, na balozi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika mkutano huo kwa lengo la kujenga ushirikiano na kutangaza ubunifu wa miradi inayoweza kufanyika Pemba.
“Tunalenga kujenga uchumi shirikishi unaozingatia uwazi, ushirikiano na mazingira rafiki kwa wawekezaji. Huu ni wakati sahihi kwa kila mmoja kuja na kuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli kwa Pemba,” alisisitiza Bw. Saad.
Wadhamini na washiriki wa maonesho wanahimizwa kujiandikisha mapema ili kufaidika na fursa za mkutano huo, ambao unatarajiwa kubadili sura ya kiuchumi ya Pemba kwa miaka ijayo.