Na Oscar Assenga,TANGA
SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) wamekutana na Mawakala wa Meli na Forodha Mkoani Tanga kwa lengo la kutoa uelewa na kukumbushana majukumu yao katika kuchangia kufanikisha ufanisi wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa njia ya Maji kutoka Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) Nelson Mlali alisema wamekutana nao ili kuwaeleza mabadiliko ambayo yanaendelea kutokea na wanachotarajia kutoka kwao na kutoa fursa ya kuweza kutoa maoni yao.
Alisema katika kikao hicho wamejikita kwenye masuala na masharti ya leseni nani anapaswa kupata leseni na anatakiwa afanye nini na asipoifuata jambo gani linaweza kumtokea wakati akiendelea kutoa huduma
Aidha alisema lengo ni kukumbusha kwenye maeneo ambayo wanadhani hawafanyi vizuri ili waweze kufanya vizuri kwa ajili ya faida ya tasnia ya usafiri kwa njia ya maji katika maeneo mbalimbali nchini
“Tunapenda kupunguza malalamiko, migogoro na ucheleweshaji wa huduma za usafiri kwa njia ya maji maana tunapochelewesha huduma labda kwa uzembe au kutokujua “Alisema
“Kwani kufanya hivyo tunazifanya bandari zetu kuwa za gharama kuliko Bandari shindani zilizopo nchi jirani tunajikuta kama nchi na kama wafanyabiashara binafasi wanapoteza na kazi nyingi zinakuwa haziji upande wetu zinaenda kwenye mataifa shindani”Alisema
Hata hivyo alitoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana kwa sababu wote wapo kwenye tasnia hiyo kutokana na kwamba wote wanafanya kazi moja ili baadae waweze kujikita kutoa huduma za usafiri kwa njia ya maji kwa ufanisi mkubwa zaidi bila kuwa na migogoro na bila kucheleweshana na kusababisha gharama kwenye mnyororo wa usafirishaji wa bidhaa na watu kwa njia ya maji .
Awali akizungumza AfisaMwandamizi wa Udhibiti Usafiri wa Njia ya Maji kutoka Shirika la Wakala wa Meli nchini Tasac Mbwana Ng’anzialisema kikubwa walichokifanya na wadau hao ni kutoa elimu na masharti ya leseni na changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza majuku yao ya kila siku.
Alisema kwamba miongoni mwa changamoto ambazo wanakumbana nazo kuchelewa kurudisha vifaa kwa wenzao jambo ambalo ni kinyume cha sheria .
Alisema wamekubaliana kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu bila kugushi nyaraka za wakala huo na kuwaeleza kuhakikisha hawafanyi hivyo ikiwemo matumizi mabaya wa fedha wanazopewa kwa ajili ya kufanya jambo Fulani.