Na Mwandishi Wetu.
MIAKA minne ya serikali ya awamu ya sita madarakani Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF),kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini umefanikiwa kuhitimisha kaya za walengwa takribani 400,000 nchi nzima baada ya kuhudumiwa kwa takribani miaka 10.
Hilo limefanikiwa kutokana na utekelezaji wa afua mbalimbali ambapo zimeboresha maisha,kuongeza rasilimali na zinaweza kuendelea kuendesha maisha yao bila ya ruzuku ya TASAF.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema hayo April 17,2025,Jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa waandishi wa habari.
Amesema kupitia mpango wa miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa hadi kufikia Disemba 2024,jumla ya miradi 27,863 ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imetekelezwa ambapo jumla ya Kaya za Walengwa 662,000 zimelipwa jumla ya shilingi bilioni 213.8.
“Licha ya kuongeza kipato, walengwa pia wameweza kupata ujuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo unaoweza kutumika katika shughuli za kukuza uchumi wa kaya na kuongeza kipato,miradi hii imenufaisha sekta za kilimo, barabara, misitu, maji na mazingira,”amesema.
Pia kupitia miradi ya kuendeleza na kuboresha Miundombinu ya Huduma za Jamii jumla ya miradi 137 ya uendelezaji miundombinu yenye thamani ya shilingi bilioni 12.67 ilitekelezwa katika Mamlaka za maeneo ya utekelezaji 29.
Kati ya hiyo miradi hiyo 6 imekamilika na 72 ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji. ambapo miradi ya aina hiyo imetatua changamoto za jamii zinazotokana na upungufu au kutokuwepo kabisa kwa miundombinu ya kutosha ya kutolea huduma za jamii katika sekta za Elimu, Afya na Maji.
“Hadi kufikia Desemba, 2024, jumla ya miradi ya jamii 1,518 yenye thamani ya shilingi bilioni 81.8 imetekelezwa ambapo miradi 659 imekamilika na inatumika kutoa huduma na miradi 859 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kupitia miradi ya Kupunguza Umaskini Tanzania-Awamu ya Nne(TPRP IV),”amesema Waziri Simbachawene.
Aidha, amesema TASAF kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) imewezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za walengwa kutambulika, kupatiwa mikopo ya elimu kwa asilimia 100 ambapo hadi kufikia Novemba 2024 jumla ya wanafunzi 8,274 wamenufaika na mikopo hii.