
Katika simulizi ya kushtua, mwekezaji kutoka Uholanzi Bi. Siriviea Vrascam amesimulia kwa uchungu namna alivyodai kuvamiwa, kupigwa, kunyanyaswa na kuporwa mali zake na watu wanaodaiwa kuwa askari – tukio lililotokea tarehe 24 Oktoba 2024 nyumbani kwake mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Bi. Vrascam amesema tukio hilo lilitokea akiwa anarejea nyumbani kwake karibu na kampuni ya kilimo ya Vasso Agroventures, ambapo ghafla alikabiliwa na watu waliovaa sare za kijeshi, ambao hawakuwa sehemu ya ulinzi wa kampuni hiyo.
“Nililazimishwa kushuka kwenye gari, wakalichukua kwa nguvu. Nilipigwa, nikadhalilishwa, na walijaribu kuninyang’anya simu niliyokuwa natumia kurekodi,” alisema kwa masikitiko. Bi. Vrascam ameeleza kuwa aliwekwa ndani ya nyumba yake kwa saa kadhaa bila msaada wowote, huku mume wake akishambuliwa na watu wengine watatu wasiojulikana na kuporwa pikipiki aliyokuwa akiitumia kutafuta msaada.
Katika usiku huohuo, anadai watu waliovaa kiraia wakishirikiana na baadhi ya askari walivamia nyumba yao, kufungua mlango kwa nguvu na kuiba mali mbalimbali ikiwemo pesa taslimu, vifaa vya kielektroniki, vito vya thamani – hadi nguo za ndani kutupwa ovyo.
“Mmoja wao alinitishia akasema, ‘Ukionekana tena na kamera, kitu kibaya sana kitakupata.’ Niliingiwa na hofu kubwa,” aliongeza kwa sauti ya kukata tamaa.
Licha ya kufungua jalada la kesi lenye namba MOS/RB/8476/024 katika Kituo cha Polisi Moshi,
Bi. Vrascam amesema zaidi ya miezi sita imepita bila hatua yoyote kuchukuliwa. Wanahabari walipojaribu kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Simon Maigwa, simu yake ilipokelewa na kaimu wake aliyedai hana taarifa kuhusu tukio hilo lakini akaahidi kulifuatilia kwa undani. Bi. Vrascam ameomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha haki inapatikana, huku akisisitiza kuwa matukio ya aina hii yanahatarisha mazingira ya uwekezaji na kuwatisha wawekezaji wa ndani na nje.